Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wananchi kujiandaa kupata chanjo ya corona kama ambavyo Waziri Mkuu Kassim Majalia ametangaza, aidha amesema kuwa marufuku mikusanyiko yote isiyo ya lazima nchi nzima na ile ambayo itaonekena ni lazima basi tahadhari zote zichukuliwe.

Hatua hiyo inalenga kukabiliana na hofu ya kuendelea kusambaa kwa mlipuko wa tatu wa janga la corona ambao tayari umeathiri mamia ya Watanzania.

Hata hivyo, agizo hilo limekuja wakati ambao tayari wakuu wa mikoa mbalimbali nchini, wakitangaza kupiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima kwenye maeneo yao.

Dkt. Gwajima amewataka viongozi wa Serikali na wa sekta binafsi kuonyesha mfano wa namna wanavyochukua hatua kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 ambapo mpaka sasa idadi ya wagonjwa wa Covid 19 imezidi kuongezeka na hadi kufikia Julai 21,2021 kulikuwa na wagonjwa 682 wanaopatiwa matibabu kwenye vituo mbalimbali..

“Ili kuimarisha zaidi kasi ya kuoambana na kudhibiti maambukizi ya UVIKO-19, natamka kuanzia leo tarehe 22/07/2021 nimekataza shughuli zote za misongamano yote isiyokuwa ya lazima . Nimekataza shughuli zote za misongamano na ile yenye ulazima tahadhari ya kutosha ichukuliwe bila kuathiri shughuli za kiuchumi na kitaifa”.amesema Dkt Gwajima

“Naelekeza wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuwapa ushirikiano waganga wakuu wa mikoa na wilaya kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Jamii Na. 1 ya Mwaka 2009 na kuweka utaratibu mzuri kwa wale wanaoomba vibali vya shughuli zenye ulazima,”amesema Dk Gwajima.

Moto wateketeza watoto wa familia moja
Gomes: Sio mchezo mdogo, nitapambana kuweka rekodi