Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameiomba serikali kupitia hazina, kurudisha kiwanda cha TABO TECHS cha Mkoa wa Tabora kutoka mikononi mwa mwekezaji na kurudishwa mikononi mwa vyama vya ushirika ili kiweze kuzalisha nyuzi za kufungia tumbaku nchini.

Ameyasema hayo leo Januari 30, 2021 alipokuwa anatoa salamu kwa Rais John Pombe Magufuli mara baada ya Rais kumaliza kuweka jiwe la msingi katika jengo la wagonjwa wa dharura katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora  na kuzindua mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda maeneo ya Tabora, Nzega na Igunga.

Bashe amesema kuwa mwekezaji wa kiwanda hicho ameshindwa kuzalisha nyuzi hizo baada ya serikali kumpa mkataba wa kuzalisha nyuzi hizo ambapo kwa mwaka serikali inanunua nyuzi hizo kutoka nje kwa dola milioni 3.2, na kwamba kwa kuzalisha wenyewe watapiga marufuku uagizwaji wa nyuzi za kufungia tumbaku kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wa Wizara ya Kilimo kwenye sekta ya kukuza uchumi wa Nchi imejiwekea malengo ya kufikia hadi asilimia 10 na pia kupunguza gharama ya fedha katika Wizara hiyo.

Aidha, ameeleza mikakati ya Bilioni 175 za Wizara hiyo kwa miaka mitano ijayo kuwa Tanzania itazalisha mbegu na kuuza kwa bei nafuu na tayari baadhi ya Mikoa mbegu za mahindi zimeuzwa kwa shilingi 5,500 kutoka shilingi 12,000 ya makampuni ya nje.

 

 

UN yatangaza udhibiti wa uuzaji chanjo
Rais Magufuli aagiza Madaktari waliohama watafutwe