Utamaduni wa uvaaji wa mavazi ulioingiliwa na mfumo wa utandawazi umepelekea uvaaji wa mavazi mafupi kwa wanawake maarufu kama ‘vimini’ na uvaaji wa mavazi wa suruali katikati ya makalio maarufu kama mlegezo kupigwa marufuku kwa kutumia kanuni na sheria ndogondogo katika maeneo mbalimbali nchini.

Jana, Uongozi wa Usharika wa Karanga wa Kanisa la Kiijili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini umetangaza kupiga marufuku mavazi ya aina hiyo kanisani.

Marufuku hiyo ilitolewa na mchungaji wa kanisa hilo, Isack Maro katika ibada iliyofanyika jana asubuhi katika kanisa hilo. Baadhi ya wachungaji na waumini waliohudhuria ibada hiyo walieleza  kuwa hawakufurahishwa na mavazi ya baadhi ya waumini.

Mchungaji huyo alisema kuwa ili kukomesha tabia hiyo, wazee wa usharika wameagizwa kuandaa khanga maalum kwa ajili ya kuwafunika wanawake wanaofika kanisani na nguo fupi. Alisema kwa kufanya hivyo, huenda wataona aibu.

“Ni lazima tujifunze kufanya mambo yanayompendeza Mungu. Tukikuona umevaa hizo nguo tutamuomba mzee wa kanisa akalete khanga au kijana umevaa mlegezo tutakutoa,” alisema Mchungaji Maro.

Baadhi ya maeneo ambayo mwanamke huishia getini akiwa amevaa nguo fupi ukiacha nyumba za ibada, ni katika hospitali ya Bugando jijini Mwanza. Uongozi wa Bugando hauruhusu mwanamke kuingia katika hospitali hiyo akiwa na kimini au suruali na mwanaume akiwa katika mavazi yasiyofaa. Pia, mwanamke haruhusiwi kuingia Bugando akiwa na nguo ambayo imeacha mabega wazi.

Kadhalika,  mbali na sheria za mavazi kwa watumishi wa umma, vipo vyuo vikuu nchini kikiwemo Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT) sheria hiyo iko wazi ambapo mwanafunzi wa kike haruhusiwi kuvaa suruari au kimini akiwa darasani. Pia, mwanaume kuvaa mlegezo au kuingia darasani akiwa na pensi.

Katika Afrika mashariki, Serikali ya Uganda ilitangaza kupiga marufuku mavazi ya vimini kwa wanawake ikiwa ni moja kati ya hatua za kulinda utamaduni na kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Dar24 Kuzindua App Mpya ya Simu Za Android, Ni zawadi Bora ya Mwaka 2015/16
Magumashi: Utashangaa Kilichomkuta Baba Wa Watoto Wawili Alipoenda Kupata Huduma Ya Tiba Mbadala