Mdau wa Soka nchini Tanzania na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Ruvu Shooting Masau Bwire, amewanasihi viongozi, wachezaji, makocha na mashabiki wa klabu ya Simba SC.

Masau ametoa nasaha kwa Wekundu wa Msimbazi kufuatia upepo mchafu unaopita kwenye klabu hiyo Kongwe, baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Masau Bwire ameandika kwenye kurasa zake za mitandao kijamii: Simba SC, nisikilizeni*…..

Naamini hamjambo?

Awali niwasihi, wale wote mlioko Dar es salaam,  na maeneo jirani, fanyeni mfanyavyo, muende uwanjani leo, uwanja wa Mkapa, mkaishangilie timu yenu katika mchezo wa ligi kuu ya NBC dhidi ya Polisi Tanzania.

Onesheni mnaipenda kweli timu yenu, mnahitaji ifanye vizuri, ipate matokeo chanya, na kwamba, yaliyopita yamepita, mnaganga yajayo, muitendee haki kaulimbiu yenu ya *Simba nguvu moja*.

Wachezaji wenu wa Simba SC,  watakapowaona kwa wingi uwanjani, watahamasika, watajua mnaipenda timu, mnawapenda pia, mnahitaji ushindi, watacheza kwa moyo na nguvu zote, ushindi utapatikana.

Msipojitokeza kwa wingi uwanjani, itawaathiri kisaikolojia wachezaji, watadhani mmewachukia, hamuwaamini tena, hamuwapendi, watacheza kwa hofu, kwamba, timu ikifungwa itakuaje, kwa hofu hiyo, usishangae wakicheza hovyo, dakika 90 zikaleta matokeo hasi Msimbazi!

Msifike huko, jitokezeni kwa wingi leo uwanjani, itakuwa sehemu ya mafanikio na ushindi kwa timu yenu dhidi ya Polisi Tanzania watakao ingia uwanjani kwa mfumo wa kukamia!

Kama kuna wakati Simba SC mnahitaji kushikamana ni sasa, wanachama, mashabiki, wapenzi na wadau wote wa Simba SC,  kama kweli mnaipenda timu yenu kwa dhati, mnapenda ushindi na mafanikio, ushindi wa mchezo wa leo ni muhimu mno, utasababisha mshikamano zaidi na ushindi wa michezo mingine ijayo ya kitaifa na kimataifa.

Nendeni uwanjani wapendwa,  kaishangilieni timu yenu, ushindi upatikane, timu ikae vizuri, heshima na hadhi yenu kisoka iendelee kushamiri, kwa kufanya hivyo na matokeo chanya kupatikana, *Simba itakuwa furaha yenu*.

Ni mtazamo tu….

Mungu ibariki Simba SC….

*Simba nguvu moja*…….

Familia ya kushangaza watoto wenye herufi za kufanana
Manara amuhofia Prince Dube