Afisa Habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire amesema kikosi chao kinaendelea na maandalizi ya Michzo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyosalia kabla ya kufikia tamati ya msimu huu 2022/23.

Ruvu Shooting tayari imeshashuka daraja, baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Simba SC majuma mawili yaliyopita, hivyo itacheza michezo miwili iliyosalia kama sehemu ya kukamilisha Ratiba ya Ligi Kuu.

Masau Bwire amesema kitakachokwenda kufanywa na kikosi chao katika michezo hiyo ni kucheza kwa heshima kwa lengo la kuiaga Ligi Kuu msimu huu, huku wakitambua mahala pao sahihi kwa msimu ujao ni Michuano ya Championship.

Kiongozi huyo amesema anaamini kushiriki kwa kikosi chao katika Ligi ya Championship ni mapenzi ya Mungu, na huenda nafasi hiyo wameipata ili kuiheshimisha Ligi hiyo ambayo imekuwa haifuatiliwi sana na Mashabiki wengi wa Soka nchini Tanzania.

“Tuna mechi mbili za Ligi kuu lakini tunajua Ligi yetu ni Championship tumeanza maandalizi na mchakato wa kuelekea mashindano hayo, pengine mapenzi ya Mungu ametupeleka huko kwa ajili ya kwenda kuihamasisha ile Ligi  kuipa hadhi na heshima, Watu wengi hawaifuatilii sasa tunataka twende ili watu wajue na huko kuna mashindano.”

“Nina imani Mungu alipenda si wengine ambao wataipa heshima na kuipa hadhi Championship bila uwepo wa Ruvu Shooting.” amesema Masau Bwire

Katika michezo ya kukamilisha Ratiba ya Ligi Kuu msimu huu 2022/23 Ruvu Shooting itacheza dhidi ya Singida Big Stars Juni 06 mjini Singida kwenye Uwanja wa Liti, na Juni 09 itamaliza na Dodoma Jiji FC katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Hersi Said: Sikujuwa kama ningekuwa Rais Young Africans
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Mei 24, 2023