Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni, amewatahadharisha wamiliki wa shule zinazotumia magari mabovu kubebea wanafunzi ikiwa ni kinyume na sheria za usalama barabarani hali ambayo inaweza kupelekea ajali.

Ameyasema hayo wakati wa Uzinduzi wa Kampeni Maalumu ya Usalama Barabarani na Udhibiti wa Ajali katika Uwanja wa Skuli ya Jang’ombe, ambapo Masauni amewataka wamiliki wa shule kuhakikisha wanatumia mabasi imara ili kuepusha ajali na kuwaasa madereva wa magari hayo kufuata sheria za barabarani.

“Nawaagiza askari wa usalama barabarani kusimamia sheria ili wamiliki watakaokiuka sharia hizo waweze kuchukuliwa hatua pamoja na madereva watakaobainika kuendesha magari mabovu ambayo ni hatarishi kwa wanafunzi,” amesema Masauni

Akitoa ripoti ya matukio ya ajali za barabarani Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Shukuru Amir Ally amesema jumla ya ajali 229 zimeripotiwa ndani ya mwaka huu tofauti na mwaka 2017 ambapo jumla ya ajali 391 zikiripotiwa huku akitoa siri ya kupungua kwa ajali hizo ni ushirikiano wanaoupata kutoka kwa wadau wa usalama barabarani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi inayojishughulisha na masuala ya usalama barabarani ya New Vision, Pily Hamis Ladya amesema kuwa wamedhamiria kufikia mikoa yote ya Zanzibar na katika awamu hii ya kwanza wanaanza na shule kumi huku akiahidi kuzifikia shule zote katika kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi.

 

Rwanda yajipanga kukabiliana na Ebola
Prof. Mbarawa azindua kampeni ya upandaji miti