Mwakilishi wa Tanzania katika Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele anatakiwa kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge, Jumatatu (Mei 20, 2019) hadi saa tano kamili, vinginevyo atakamatwa na kufikishwa kwenye kamati hiyo.

Kauli hiyo imetolewa jana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai alipokuwa akizungumzia kile alichokieleza kuwa ni ukaidi wa mbunge huyo ambaye pia ni Mbunge wa Shinyanga Mjini kwa tiketi ya CCM, baada ya kumuita arejee nyumbani kutoka Afrika Kusini alikokuwa anahudhuria vikao vya PAP.

“Mwisho ni Jumatano saa tano asubuhi,” alisema Ndugai. “Awe amefika, na ikiwa hajafika itatolewa hati ya kukamatwa. Kwa sasa bado ni mtu wa kawaida,” aliongeza.

Spika Ndugai ameeleza kuwa Masele amekuwa akichonganisha mihimili kwa kutoa kauli zisizo za kweli pamoja na kufanya mambo aliyoyaelezea kuwa ni ya hovyo-hovyo katika Bunge la Afrika.

Masele ambaye ni Makamu wa Rais wa PAP, aliunda tume maalum ya kuchunguza tuhuma za ngono, rushwa na matumizi mabaya ya ofisi amesema kuwa tume hiyo imeshakamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti.

“Rais Dang anajua misimamo yangu kama makamu wa kwanza wa Rais na sipendi mambo ya hovyohovyo, akaamua kumtumia Spika wetu wa nyumbani aweze kuniita haraka nyumbani ili nisiwepo Afrika Kusini nisiweze kuongoza vikao ambavyo vingejadili ripoti ya uchunguzi huo,” alisema Masele alipozungumza na DW.

Spika Ndugai ameeleza kuwa anao uwezo wa kusitisha ubunge wa Masele kwenye Bunge la Afrika endapo ataendelea kuwa mkaidi kwani Bunge la Tanzania ndilo lililomtuma. Alisema ambacho hawezi kufanya ni kusitisha ubunge wake wa Shinyanga ambao alichaguliwa na wananchi.

Masele amesikika akieleza kuwa ataitikia wito huo na kwamba baada ya kuhojiwa na Kamati ya Bunge atazungumza na waandishi wa habari.

UVCCM waanika siri watakayoitumia kumng’oa Msigwa Iringa Mjini
Kenya ‘yalamba dili’ kufundisha Kiswahili shule za Afrika Kusini

Comments

comments