Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Ufaransa Didier Deschamps amesema hali ya Kambi ya kikosi chake ni Shwari, kuelekea mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Dunia dhidi ya Australia utakaopigwa baadae leo Jumanne (Novemba 22) nchini QATAR.

Mashabiki wa Soka wa Ufaransa wamekua na wasiwasi kuhusu hali ya kikosi chao, baada ya kuondolewa kwa Mshambuliaji Karim Banzema mwishoni mwa juma lililopita, kufuatia majeraha yanayomkabili kwa sasa.

Mbali na Benzema, Ufaransa pia itawakosa wachezaji wengine kama Christopher Nkunku, Presnel Kimpembe, N’Golo Kante na Paul Pogba.

Kocha Deschamps amesema wachezaji waliopo kikosini kwa sasa wapo katika hali nzuri na wamedhamiria kupamban ili kupata ushindi utakaowaongoza katika safari yao ya kutetea taji la Dunia.

“Hakuna wasiwasi. Tumefanya kila linalowezekana, kila mtu ametulia, tunasubiri mchezo wetu dhidi ya Australia, ambao tunatarajia utakua na upinzani mkubwa kutokana na wenzetu kujiandaa kama tulivyojiandaa.”

“Roma haikujengwa kwa siku moja, haiwezi kutokea mara moja, lakini tuna kile tunachohitaji. Tuna wachezaji wa kutosha ambao wanaweza kuamsha, kuwafanya wengine kwenda, kuzungumza kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.”

“Ni muhimu kwamba kila mchezaji anapaswa kuwa kiongozi katika nafasi yake, kisha tutaona matokeo baada ya mchezo.”

Benzema, ambaye ni mshindi wa Ballon d’Or 2022, aliondolewa baada ya kupata jeraha la paja wakati wa mazoezi na Ufaransa na Deschamps amechagua kutomwita mbadala wake.

“Nina wachezaji 25 kwenye kikosi changu. Nina uhakika nina idadi nzuri ya wachezaji wa kuweza kukabiliana na changamoto zinazotukabili,” alisema Deschamps kuhusu uamuzi wake.

“Kabla ya kuanza kwa Fainali hizi tulikuwa na wachezaji 22 hadi 23, kisha wakafika 26 na sasa tumebaki na wachezaji 25. Kuna uwezekano mkubwa wachezaji waliobaki wakashangaza, ndio maana sikutaka kumuongeza mwingine.” amesema Deschamps

Mchezo wa Ufaransa dhidi ya Australia umepangwa kuanza mishale ya saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Ubelgiji yakubali yaishe, kutumia jezi nyekundu
Lionel Messi: Hii ni nafasi yangu ya mwisho