Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo dos Santos Aveiro, amewaweka njia panda mashabiki wa soka wa nchi hiyo, baada ya kushindwa kuweka wazi mustakabali wake wa kuendelea kuitumikia The Navigators.

Ronaldo ameibua hofu kwa mashabiki wa soka nchini Ureno, kufuatia  kauli tata aliyoitoa siku moja baada ya timu ya taifa hilo kuondolewa kwenye fainali za kombe la dunia kwa kufungwa mabao mawili kwa moja na Uruguay, katika mchezo wa hatua ya 16 bora.

Mshambuliaji huyo wa klabu ya Real Madrid alipohojiwa na vyombo vya habari aliwashukuru mashabiki kwa mchango wao mkubwa waliouonyesha wakati wote walipokua wakishiriki fainali za kombe la dunia, hadi walipotolewa juzi jumamosi.

Alipotakiwa kuweka wazi mustakabali wake baada ya Ureno kushindwa kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa dunia, Ronaldo alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo na badala yake akawataka waandishi wa habari waridhike na salamu za kuwashukuru mashabiki alizozitoa.

“Sina jambo lingine la kusema zaidi ya kuwashukuru mashabiki wetu, wamejitolea kuja hapa kutushangilia tangu mwanzo hadi tumeondolewa kwenye michuano hii, Ninawashukuru sana.

“Siwezi kusema lingine lolote, zaidi ya kutoa shukurani kwa mashabiki.”

Alisisitiza Ronaldo baada ya kuulizwa mustakabali wake ndani ya kikosi cha timu ya taifa ya Ureno.

Ronaldo kwa sasa ana umri wa miaka 33, hali ambayo inaendelea kuzua hofu kwa mashabiki wa soka wa Ureno kwa kuhisi huenda akatangaza kustaafu soka la kimataifa kutokana na sababu za umri.

Ni dhahir mshambuliaji huyo hatoweza kuwa miongoni mwa wachezaji watakaocheza fainali za 2022 zitakazochezwa nchini Qatar, kwani kwa wakati huo atakua amefikisha umri wa miaka 37.

Zlatko Dalic: Luca Modric ni nahodha asiyekata tamaa
Video: Madude kumi yaliyomng'oa Mwigulu, Utabiri wa Lema watimia, Nape, Zitto wamkaribisha uraiani