Mfadhili wa zamani wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC, Azim Dewji amesema ameamua kutumia Shingili milioni 20 kununua Flana (Tshirt) atakazozigawa kwa Vijana 2000 watakaoishabikia Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakapocheza dhidi ya DR Congo katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la Dunia 2022.

Stars itakuwa mwenyeji wa DR Congo keshokutwa Alhamis (Novemba 11) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, katika mchezo wa mzunguuko wa tano wa Kundi J.

Dewji amewataka Watanzania na Wadau wa soka kushirikiana kwa pamoja kuiunga mkono Taifa Stars katika mchezo huo na kuongeza kuwa, atazikabidhi jezi hizo TFF ambapo watazigawa kwa vijana hao 2000 ambao wataenda uwanjani kuipa nguvu Taifa Stars, pia atatoa tiketi 100 kwa ajili ya Wafanyakazi wake kwenda uwanjani.

“Tubadilike hii ni Timu yetu hatuombi pesa maana Waziri Mkuu ameshakusanya pesa na amepata za kutosha na Mama naye amesema ana imani na Timu, tumebakia sisi Wapenzi na Mashabiki kwamba lazima na sisi tuige na tufate yale yaliyozungumzwa na Viongozi wetu, tunaomba siku ya alhamis tuwape ruhusa Watanzania wakaishabikie Timu yetu.” amesema Azim Dewji

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya GSM Gharib Said Mohamed (GSM) amenunua tiketi mia tano na kuzigawa bure kwa Mashabiki kwa ajili ya mchezo wa Taifa Stars dhidi ya DR Congo.

Gharib amechukua maamuzi hayo kwa ajili ya kutoa nafasi kwa Mashabiki kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa keshokutwa Alhamisi (November 11) Kuisapoti Taifa Stars ambayo inahitaji ushindi katika mchezo huo.

Taifa Stars inaongoza Msimamo wa Kundi J, ikiwa na alama 7 sawa na Benin inayoshika nafasi ya pili, DR Congo ipo nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 5 na Madagascar inaburuza mkia ikiwa na alama 3.

Hitimana: Nitashirikiana na Franco Pablo Martin
Yericko asitisha kuishtaki Young Africans