Mashabiki na Wanachama wa Young Africans wameombwa kufika kwa wingi Uwanja wa Taifa kesho Jumatano, kwa lengo la kuipa nguvu timu yao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, dhidi ya Namungo FC.

Ombi hilo kwa Mashabiki na Wanachama limetolewa na uongozi wa klabu hiyo, huku kiingilio cha chini kikiwa shilingi 5000.

Kikosi cha Young Africans hakijapata ushindi katika michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu ambayo ni dhidi ya JKT Tanzania waliyotoka sare ya bao moja kwa moja, kisha kikaambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Azam FC.

Afisa Mhamasishaji wa Young Africans, Antonio Nugaz  amesema viingilio vya mchezo wa kesho  VIP A  kitakuwa Shilingi 15,000 wakati VIP B na C kiingilio kitakuwa Shilingi 10000.

Nugaz amewataka Mashabiki na Wanachama kufika kwa wingi katika mchezo huo utakaoanza saa 1:00 usiku ili kuiunga mkono timu yao, huku akiwasisitiza kuzidi kujilinda na maambukizi ya virusi vya Corona kwa kuvaa barakoa.

“Maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yanakwenda vizuri huku tukiamini tutapata ushindi. Niwaombe mashabiki waje kwa wingi uwanjani kuiunga mkono timu yao, najua kuna mambo mengi yametokea baada ya mechi na Azam  na kupelekea baadhi  kuwa na hasira na kuwashutumu wachezaji lakini niwaombe tuwe na subra na tuzidi kuwapa moyo wachezaji wetu ili tumalize mechi zilizobaki vizuri” amesema Nugaz.

Nugaz amesema kuwa ni jambo la busara kwa Mashabiki na Wanachama wa Young Africans kuungana kwa sasa ili timu ifanye vizuri.

“Muhimu ni Mashabiki, Wanachama kuungana na kuisapoti timu ili tumalize vizuri mechi zilizobaki halafu sasa ndio tunaanza kujipanga kwa msimu ujao, ambao utakuwa msimu wa kishindo na natumaini.”

“Wakati mwingine muungwana akifanya lake na kuona haliendi vizuri anatulia na kujitathimini, na matatizo kwenye timu ni jambo la kawaida kwani hata hao wachezaji wanaolalamikiwa huko walikotoka walikuwa wanafanya vizuri lakini wamekuja hapa hawafanyi vizuri na hiyo ni sehemu ya mchezo.”

“Tunatakiwa kuendelea kuwasapoti na kuwapa moyo, kwani hata Obrey Chirwa alikuwa hapa na baadhi wakamuita garasa lakini baadae akawa tishio ” amesema Nugaz.

Young Africans ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ku kwa kufikisha alama 56 ikifuatiwa na Namungo FC yenye alama 54.

Timu hizo zilipokutana kwenye mzunguuko wa kwanza msimu huu 2019/20, Majaliwa Stadium mjini Ruangwa mkoani Lindi zilitoka sare ya bao moja kwa moja.

TAKUKURU yawatia mbaroni wafanyakazi 30 wa MSD
Mahujaji wachache kuingia Saudi Arabia mwaka huu