Waziri wa Nishati, January Makamba amewataka watu wenye uwezo wa kujenga vituo vya Mafuta Vijijini kufika Wizarani kwa ajili ya kupatiwa maelekezo ili waweze kufanikisha zoezi hilo na kuwasaidia Wananchi wa maeneo hayo kupata mafuta safi.

Makamba ameyasema hayo katika Kata ya Buselesele iliyopo Jimbo la Chato katika siku ya tano ya ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi juu ya umeme, wakati akizungumza na Wananchi wa eneo hilo pamoja na wa Jimbo la Busanda.

Amesema kwa sasa Serikali imepunguza masharti ya kujenga vituo vya mafuta, na kusema maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassani ni kuhakikisha mafuta safi yanapatikana nchi nzima ili kuachana na mafuta ya kwenye vidumu.

Waziri wa Nishati, January Makamba.

Katika upande mwingine Waziri Makamba amesema Serikali kwasasa inakopesha pesa kwa yoyote anayetaka kujenga kituo cha Mafuta Kijijini na masharti ya kujenga vituo hivi yamelegezwa.

“Kwasasa ukiwa na Milioni 40 unajenga kituo, watu waje wakope hizi pesa, maana tumetenga Bilioni 2 kwa ajili ya watu kukopeshwa na lengo la Rais samia ni kuhakikishabmafuta safi yanapatikana nchi nzima,” amefafanua Waziri Makamba.

Ziara ya Waziri huyo wa Nishati, January Makamba inaendelea katika ukanda wa ziwa Vitoria na sasa ipo Mkoani Kagera, baada ya kupita mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza na Geita.

Habari kuu kwenye magazeti ya leo Julai 16, 2022
UN yaalaani mauaji watu 22 Ukraine