Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amefungua mashindano ya Utamaduni yanayohusisha ngoma na vyakula vya asili Tanzania Bara na Visiwani.

Gekul amefungua mashindano hayo hii leo Julai 1, 2022 jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Uhuru na kuesema Wizara hiyo imejipanga kuendeleza mashindano hayo ili yafayike kila mwaka.

“Leo ni siku ya kipekee, hili ni tukio la kihistoria, ni mara ya kwanza tamasha hili la kitaifa kuandaliwa, tamasha la mwaka huu ni mwanzo wa kufanyika kwa matamasha haya nchi nzima kwa kuzunguka Mikoa yote, muioneshe dunia kuwa Tanzania ni tajiri wa Utamaduni na umahiri wake,” amesema Gekul.

Hata hivyo, Waziri Gekul amesisistiza kuwa tamasha la mwaka 2023, litaandaliwa na taarifa zake kutangazwa mapema ili mashindano hayo yaanzie katika ngazi ya Kata, Wilaya, Mkoa na Kitaifa.

Awali wakati akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mashindano hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Saidi Yakubu amesema tamasha la kwanza la Utamaduni la Kitaifa litaendelea tena Julai 2, 2022.

Amesema tamasha hilo litaanza kwa matembezi yatakayopokelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye atanarajiwa kulizindua rasmi tamasha hilo.

Aidha Yakubu ameongeza kuwa, Julai 3, 2022 Wizara hiyo imeandaa usiku wa taarabu ambao umebeba sura ya Kimataifa kwa kuhusisha vikundi vya Taarabu kutoka nchi za Burundi, Kenya na Visiwa vya Comoro.

Tuzo 2021/22 kutolewa Julai 07 Dar es salaam
Neymar aichoka PSG, atamani soka la England