Aliyekua kocha msaidizi wa mabingwa wa soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba, Masoud Djuma ameonesha kushangazwa na tetesi zinazomuandama za kuwa mbioni kujiunga na Young Africans.

Jana jioni, uongozi wa klabu ya Simba ulithibitisha kuvunja mkataba wa kocha huyo kutoka nchini Burundi, baada ya mazungumzo ya muda mrefu ambayo yalishindwa kupata muafaka wa tatizo linalotajwa kuwa kwenye benchi la ufundi la klabu hiyo.

Djuma anadaiwa hakuwa na mahusiano mazuri na Kocha Mkuu, Patrick Aussems, hali ambayo ilitajwa kuwa chanzo cha baadhi ya wachezaji kuanza kujenga makundi baina yao.

Baada ya kuthibishwa anaondoka Simba, Djuma alizungumza na Dar24 kwa njia ya simu, na tulipomuuliza kuhusu ukweli wa safari yake ya kwenda Young Africans alijibu kwa mshangao, “Sijui mnatoa wapi mambo ya Yanga, mimi najua Yanga ina kocha wake, wako wasaidizi wake.”

“Sasa mimi naenda vipi Yanga, kukaa wapi pale?” Alihoji.

Hata hivyo, kocha huyo aliyejiunga na Simba Oktoba mwaka jana, amesema bado yupo jijini Dar es salaam na atakapokua tayari kuondoka atafanya tendo la kiungwana na kuagana na watu wake wa karibu wakiwemo waandishi wa habari.

“Bado nipo Dar es Salaam, nikitaka kuondoka nitaaga maana sijaiba wala sina ugomvi na mtu,” aliiambia Dar24.

Kocha huyo aliyewahi kuinoa Rayon Sports ya Rwanda kwa mafanikio makubwa, amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba. Wengi wameonyesha kutofurahishwa na kuondoka kwa Djuma ambaye kabla alikuwa chini ya Mfaransa, Pierre Lechatre.

Djuma aliwahi kuwa kocha mkuu katika michezo mitatu ya ligi kuu kwa mwezi mmoja kati ya Desemba 30 na Januari 27, ambapo alishinda michezo yote (dhidi ya Ndanda, Singida na Kagera), pia aliiongoza Simba kwenye mechi 4 za Kombe la Mapinduzi.

Buffon atangaza njaa ya miaka 10 ijayo
Maajabu mapacha kuolewa na mwanaume mmoja

Comments

comments