Hali si shwari ndani ya FC Barcelona kufuatia washambuliaji Lionel Messi na Antoine Griezmann kutibuana mazoezini na kumfanya kocha wao Quique Setien kuingilia kati kuweka mambo sawa.

Taarifa iliyoripotiwa na tovuti ya Diario Gol ya huko Hispania imedai kuwa Messi na Griezmann walitibuana kwenye mazoezi ya timu hiyo na kumfanya kocha wao Setien na wachezaji wengine wa timu hiyo kuingilia kati ili wasirushiane ngumi.

Hata hivyo wawili hao inasemekana wamekua na tofauti za muda mrefu, na kwenye mchezo dhidi ya Leganes, Messi aliripotiwa kutompasia Griezmann hata mara moja.

Wakati Griezmann akionekana huenda akafunguliwa mlango wa kutokea, Messi anaripotiwa kukaribia kusaini dili jipya litakalomfanya kuendelea kubaki Nou Camp kwa muda mrefu zaidi.

Griezmann ameshindwa kuonyesha kiwango bora tangu alipotua FC Barcelona kwa ada ya Pauni milioni 108 akitokea Atletico Madrid kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.

FC Barcelona kwa sasa inatazama namna ya kupunguza bili ya mishahara kwenye kikosi chao baada ya janga la Corona, huku hesabu zikipigwa za kumpige bei staa huyo wa Ufaransa.

Manchester United walihusishwa juu ya kumsajili Mshambuliaji huyo wa ufaransa kabla ya kwenda kujiunga na FC Barcelona, huku kinachosemwa ni kwamba miamba hiyo ya Old Trafford inaweza kuihitaji tena saini yake kama wakisikia amewekwa sokoni.

Waliosaidia kukamatwa karafuu Pemba kupewa motisha
Hofu yatawala Manchester City