Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo duniani (FAO), na mfuko wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo (IFAD), wameonya kwamba Mataifa mengi ulimwenguni yanarudi nyuma badala ya kusonga mbele katika jitihada za kutokomeza njaa na utapiamlo.

Onyo hilo, limetolewa na mashirika hayo jijini Roma Italia wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa la muongo wa Umoja wa Mataifa wa kilimo cha familia (2019-2028-UNDFF), linalofanyika kwa njia ya mtandao uliofanyika hapo jana Septemba 19 na unaotarajia kumalizika Septemba 22, 2022.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mkurugenzi mkuu wa FAO, QU Dongyu amesema idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa iliongezeka mwaka 2021, na inakabiliwa na hatari ya kuongezeka zaidi hasa miongoni mwa walio hatarini zaidi, ambao karibu asilimia 80 wanaishi vijijini na ni wakulima wadogo wa familia.

Watoto wakipata lishe bora, huwa na furaha na huepukana na maradhi mbalimbali. Picha na WHO.

Amesema, “Wakulima wa familia wanapaswa kuwa katika kitovu cha juhudi za kubadilisha mifumo ya chakula na kilimo ikiwa tunataka kufanya maendeleo ya kweli katika kutokomeza njaa, Kilimo cha familia ndiyo njia kuu ya kilimo katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea na ina jukumu la kuzalisha asilimia 80 ya chakula cha dunia.”

Aidha, amebainisha kuwa pamoja na kwamba wao ndio wazalishaji wa chakula lakini mara nyingi, wakulima hao wa familia wanahaha kulisha familia zao wenyewe huku kilimo cha familia kikikuza sera jumuishi na uwekezaji kwa wakulima na FAO kusaidia utekelezaji wa zana na miongozo ya kimataifa ya kuimarisha kilimo hicho.

Katika kongamano hilo la pamoja kati ya FAO na IFAD, wadau walitumia fursa ya kutoa maoni mbalimbali na kufanya majadiliano ili kubaini sera za kipaumbele na maeneo ya kiufundi ambayo yataunda ajenda ya UNDFF kwa kipindi kijacho cha utekelezaji, na kusaidia kwa ufanisi zaidi wakulima wa familia duniani kote.

Rais Mwinyi 'ateta' na Balozi wa Australia
Serikali: Makusanyo ya tozo yamesaidia huduma za Msingi