Jeshi la Polisi kitengo cha Kuzuia na Kupambana na  Dawa za Kulevya (ADU) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kukutwa na pakiti 13 za dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilogramu 30.6.

Taarifa za kushikiliwa kwa watuhumiwa hao zimetolewa mkoani Dar es salaam na mkuu wa kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Kamishna Msaidizi wa polisi Kabakele Salim Hassan wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema katika upekuzi uliofanywa katika nyumba za watuhumiwa hao, pia wamekutwa na  dola elfu 14 za Kimarekani, zaidi ya shilingi milioni 12 pamoja na misokoto mitatu ya bangi.

Katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu, Jeshi la Polisi kitengo cha Kuzuia na Kupambana na  Dawa za Kulevya limekamata watu 832 wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Baada ya kuhojiwa, watuhumiwa hao wamekiri kujihusisha na biashara hiyo haramu, na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 10, 2021
Francis Baraza anukia Kagera Sugar