Vurugu zimeibuka katika ukumbi wa Bomas ambao unatumika kutoa matokeoa ya Urais nchini Kenya, ambapo Polisi na vyombo mbalimbali vimeingia kati na kuamulia ugomvi ikiwa ni dakika chache baada ya Mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, Wafula Chabukati kuingia ukumbini.

Baadhi ya watu walianza kurushiana ngumi na kutupiana viti kwa sababu ambazo bado hazijafahamika huku ikidaiwa kuwa Mgombea wa Urais wa Azimio Raila Odinga amegoma kuingia ndani ya ukumbi huo hadi pale mawakala wake watakapopatiwa matokeo na kujiridhisha na kwamba imearifiwa kwamba kuna mambo ambayo bado hawajakubaliana na hivyo haitawezekana kutoa matokeo.

Askari wakiamua vurugu ndani ya ukumbi wa Bomas nchini Kenya.

Awali, matokeo hayo walikuwa yatangazwe muda wa saa tisa alasiri, lakini yaliahirishwa hadi muda wa saa kumi jioni, ambapo mpaka tunachapisha Habari hii bado hakuna muafaka wa matokeo hayo na tayari matangazo ya luninga ya moja kwa moja yamekatwa kwa muda.

Kenya, ilifanya uchaguzi wake wa kitaifa Agosti 9, 2022 ambapo mpaka matokeo yanatarajia kutangazwa hii leo Agosti 15, 2022 wagombea wawili yaani Raila Odinga na William Ruto walikuwa wanachuana vikali na kura zao zilikuwa hazijapishana kwa kiwango kikubwa.

Matokeo Kenya: Hali ya utulivu yarejea matokeo yaanza kutolewa
Takwimu sensa kusaidia tathmini za Wafanyabiashara