Mabingwa wa Kombe la Shirikisho (ASFC), Simba SC wamesema walistahili kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa sababu ya “kufaulu” kupita kwenye “njia ngumu” kuanzia hatua ya kwanza.

Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema kuwa safari ya kutwaa ubingwa huo kwao ilikuwa ngumu, na ubora wa kikosi chao ndio umefanikisha kuibuka washindi wa taji hilo la tatu msimu huu.

Matola amesema walikutana na ushindani mkubwa kuanzia mchezo wao wa kwanza, huku wakiziondoa AFC Arusha, Mwadui FC, Stand Utd, Azam FC, Young Afrcans na kumaliza na Namungo FC kwenye mpambano wa fainali.

Matola Amewapongeza wachezaji wa Simba kwa kupambana na kusaka ushindi katika kila mchezo wa michuano hiyo msimu wa 2019/20 waliyocheza, ingawa baadhi ya michezo hawakuonyesha ubora wao kutokana na changamoto tofauti walizokutana nazo.

Hata hivyo kocha huyo Ameutaja mchezo ujao wa Ngao ya Hisani dhidi ya Namungo FC, kwa kusema hautakuwa mwepesi kwa sababu wanakutana na timu moja kwa mara ya tatu ndani ya muda mfupi.

“Tumewafunga mara mbili, naamini nao wametusoma na hawataingia uwanjani kama michezo iliyopita, tutarajie mchezo mwingine bora na wenye ushindani,” Matola alisema.

Kocha huyo mzawa ameongeza kuwa msimu ujao utakuwa na ushindani zaidi kwa sababu kila timu imejipanga kuboresha kikosi chake na kutorudia makosa waliyofanya kwenye msimu uliomalizika Agosti 02.

Kwa upande wa nahodha na mshambuliaji wa kikosi cha Simba SC, John Bocco, amesema wanawashukuru mashabiki wao kwa kuwaunga mkono katika michezo yao yote waliocheza, licha ya baadhi ya michezo hiyo walipata matokeo ya kuumiza.

Bocco amesema michezo yote waliocheza ilikuwa na ushindani mkubwa, na wachezaji waliingia uwanjani kupambana na hatimaye wamemaliza msimu kwa kuchukua mataji yote matatu.

“Asante Mungu, tulianza kwa ubingwa na kumaliza kwa ushindi, tunaahidi msimu ujao pia tutaendelea kufanya kazi nzuri, tunawaambia mashabiki wetu tuendelee kushirikiana ili kufikia malengo, umoja na ushirikiano ni vitu muhimu katika klabu,” Bocco amesema.

Jumapili Agosti 02 Simba SC walitwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho (ASFC) baada ya kuifunga Namungo FC mabao mawili kwa moja, shukrani magoli yaliyowekwa kimiani na Luis Miquissone na Bocco wakati bao pekee la wapinzani wao lilifungwa na Edward Manyama.

Jaji Mutungi awaasa CHADEMA kutii sheria za nchi
Mwenyeji wa Fainali ASFC kutuma maombi TFF