Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Seleman Matola amemtaka Mlinda Lango chaguo la Pili Beno David Kakolanya kuendelea kupambana, ili kumpa changamoto ya ushindani Mlinda Lango chaguo la Kwanza Aishi Salum Manula.

Beno amekua mlinzi wa lango la Simba SC katika michezo minne mfululizo ya Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold, Mbeya City, KMC FC na Mtibwa Sugar, huku akipata nafasi kama hiyo kwenye michezo ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ msimu huu.

Kocha Matola ameonesha kumuamini sana Mlinda Lango huyo, ambaye ameonesha uhodari mkubwa kwenye michezo aliyocheza tangu kocha huyo mzawa anayekaimu nafasi ya Kocha Mkuu baada ya kuondoka kwa Pablo Franco Martin, kuanza majukumu yake kama Mkuu wa Benchi la Ufundi.

Baada ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar leo Alhamis (Juni 23) uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Matola alisema Beno ni kipa mzuri na mwenye viwango, lakini anapaswa kuendelea kudhihirisha hilo ili kuongeza changamoto ya ushindani dhidi ya Manula.

“Beno ameonyesha uwezo mkubwa sana tangu nilipoanza kumpa nafasi, ninafurahishwa na mwenendo wake kwa kweli. Anatakiwa kuendelea hivi ili kumpa changamoto Aishi.”

Pia wachezaji wengine niwapongeze wameonyesha uwezo mkubwa sana katika mchezo wetu wa leo, ninaimani tutaendelea kupambana hadi katika mchezo wa mwisho na kupata matokeo mazuri. alisema Kocha Matola

Simba SC imeifunga Mtibwa Sugar mabao 2-0, na kufikisha alama 60 zinazoendelea kuiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 70 kileleni.

Mtibwa Sugar yenye alama 31, imeendelea kushika nafasi ya 12 ikisaliwa na michezo miwili dhidi ya Namungo FC Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro, kisha itamaliza msimu kwa kucheza na Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Simba SC itamaliza michezo yake ugenini dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kisha watapambana na Mbeya Kwanza FC kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.

Habari kuu kwenye magazeti ya leo Juni 24, 2022
Kocha Mtibwa Sugar aukubali uwezo wa Sakho