Kiungo wa klabu ya Arsenal Matteo Guendouzi anaamini klabu hiyo ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu, licha ya kuanza vibaya kwa kufungwa na mabingwa watetezi Man City mwishoni mwa juma lililopita.

Guendouzi mwenye umri wa miaka 19, amesema haoni sababu ya kushindwa kufikia lengo la kutwaa ubingwa mwishoni mwa msimu huu, kutokana na kikosi chao kuwa na kila sababu ya kufanya hivyo.

Kiungo huyo aliyejiunga na Arsenal miezi miwili iliyopita akitokea klabu ya Lorient kwa ada ya Pauni milioni 7, amesema lengo kubwa kwa sasa klabuni hapo  ni kutorejea makosa yaliyofanywa misimu kadhaa iliyopita, na kilicho mbele yao ni kuhakikisha wanafanya vizuri na kurejesha heshima iliyopotea tangu msimu wa 2003/04.

“Ndio, ninaamini tunaweza kutwaa ubingwa msimu huu, kwa sababu tuna kila sababu ya kufanya hivyo,” Alisema Guendouzi baada ya kuhojiwa na mwandishi wa gazeti la The Standard.

“Hakuna kinachotuzuia kufanya hivyo, kwa sasa Arsenal ina kikosi bora, kinachoweza kupambana na klabu yoyote ndani na nje ya England, sina shaka na haya ninayoyasema.”

“Suala la kuanza vibaya kwa kufungwa na Man City, ni jambo la kawaida na kila mmoja hakulitegemea hilo, lakini tumejifunza mengi kupitia mchezo huo, ninatarajia makubwa na mazuri yanakuja siku za karibuni.”

Guendouzi aliripotiwa kuzikataa ofa za klabu kama PSG (Ufaransa) na Borussia Dortmund (Ujerumani), na inasadilikiwa shughuli ya kushawishiwa kujiunga na Arsenal ilifanywa na aliyekua mshambuliaji wa klabu hiyo ya kaskazini kwa jijini London Jeremie Aliadiere, ambaye ni mtu wake wa karibu.

Lakini alipoulizwa kuhusu tetesi hizo, alikiri kuwa na ukaribu na mshambuliaji huyo aliyekua naye kwenye klabu ya Lorient ya Ufaransa, na alihusika katika harakati za safari yake ya kuelekea kaskazini mwa London.

“Nilizungumza na Jeremie kuhusu Arsenal, aliniambia ni mahala salama kwangu hasa ukizingatia umri nilio nao, nilifanya maamuzi ya kuja hapa, ninashukuru uwezo wangu umeanza kuonekana na kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza.”

“Ukweli klabu ya Arsenal ilikua moyoni mwangu kwa kipindi kirefu, nilitafuta ushauri kwa makusidi ya kujiridhisha kama ningeweza kuwa katika mahala salama, nilipokua mdogo nilikua shabiki mkubwa sana wa mshambuliaji Thierry Henry na ndiye alinivutia kuipenda klabu hii.”

Mbali na mchezo wa ufunguzi, Matteo Guendouzi alikua kivutia wakati wa michezo ya kujiandaa na msimu mpya, ambapo Arsenal walipambana na Atletico Madrid, PSG, Chelsea na SS Lazio mwezi uliopita.

Video: Walimpiga kwasababu alifanya fujo- IGP Sirro
RC Chalamila aamuru Jeshi la Polisi kuwasweka ndani wananchi Kijiji kizima