Mauaji yaliyotokea nchini Burundi mwishoni mwa wiki iliyopita ambayo yanatajwa kuwa makubwa zaidi tangu Aprili mwaka huu, yamepelekea baadhi ya raia na maafisa wa Marekani kukimbia  nchi hiyo.

Ijumaa ya wiki iliyopita, watu 87 waliripotiwa kuuawa mjini Bujumbura katika machafuko makubwa yaliyofanyika usiku.

Mauaji hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki yalitokana na uvamizi wa kambi za majeshi ya nchi hiyo yaliyofanywa na watu wanaopinga serikali ya rais Pierre Nkurunzinza ambaye anadaiwa kuwa chanzo cha machafuko hayo baada ya kugombea muhula wa tatu kinyume cha katiba ya nchi hiyo.

Mwezi uliopita nchi nyingine zikiwemo Ubelgiji ziliwashauri raia wake kuondoka nchini humo huku Umoja wa Ulaya ukipunguza idadi ya watumishi wake pamoja.

“Kufuatia machafuko ambayo yanaendelea kuongezeka, Wizara ya Kigeni imeagiza kuondoka kwa jamaa za maafisa wa Marekani na maafisa ambao si wa kushughulikia dharura nchini Burundi,” taarifa rasmi ya Marekani ilisema.

Tayari shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetangaza kuanza uchunguzi dhidi ya mauaji hayo.

Chanzo: BBC

Safari za Madiwani Zafutwa, Watakiwa Kutembelea Vijiji
Aliyekosoa chama tawala Kufungwa Jela Miaka Nane