Mavuno ya zao la pamba yanatarajia kupanda nchini hadi kufikia tani 250,000 katika mwaka 2015/2016.

Kiasi hicho cha mavuno ni ongezeko kubwa kulinganisha na tani 148,000 zilizopatikana katika mwaka 2014/2015 kutokana na hali mbaya ya hewa iliyojitokeza wakati wakulima wakiendelea kutunza zao hilo.

Kufuatia matarajio hayo, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Gabriel Mwalo amewataka wakulima kuzingatia kilimo cha kisasa na rafiki kwa mazingira. Aliwataka wakulima hao kujiandaa kukabiliana na madhara yatakayotokana na mvua za El Nino.

Mkurugenzi huyo wa TCB aliwataka wakulima kuandaa mazingira bora ya ardhi kwa kufanya kilimo cha mzunguko pamoja na kupanda miti inayoongeza rutuba na kulinda ardhi ‘jatropha’ kama sehemu ya mikakati ya kupambana na mvua kubwa inayotarajiwa.

Ongezeko la mavuno ya Pamba yanayotarajiwa ni habari njema kwa wakulima ambao wengi wanatarajia kunufaika na ahadi ya viwanda vya uzalishaji nguo vitakavyoongeza thamani ya zao hilo nchini, iliyotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni.

Rais Magufuli aliahidi kufufua viwanda vya pamba na kujenga viwanda vingine vipya vitakavyosaidia katika uzalishaji wa nguo zitakazouzwa ndani na nje ya nchi badala ya pamba kuuzwa kama malighafi katika nchi za nje.

 

Muhimbili Yalaani Kilichofanywa na Waandishi Wa Habari, Rais Magufuli Alipofanya Ziara ya Kushtukiza
Wenger Alamba Tuzo England