Mawakili wanaotoa  msaada wa kisheria kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali yakiwamo ya jinai, wameshauriwa kutekeleza  jukumu hilo kwa kuzingatia weledi wa taaluma zao na si vinginevyo.

Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria,  Profesa  Sifuni Mchome katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili  Tanganyika ( TLS) muda mfupi baada ya  Ujumbe wa Makatibu Wakuu kumaliza  mazungumzo yao na  mahabusu na wafungwa  wanaume na  wanawake waliopo katika Gereza la Bukoba.

Ushauri huo umetokana na kisa cha mahabusu mmoja ambaye amekaa  ndani ya  gereza hilo kwa zaidi ya miaka sita akisubiri kukamilika kwa upepelezi wa tuhuma za mauaji anazokabiliwa nazo.

Mahabusu huyo  aliwaeleza  Makatibu  Wakuu hao, kwamba licha ya yeye kuwa tayari kukiri kosa lake na alikuwa tayari kufanya hivyo, lakini  Wakili  aliyekuwa anamsimamia alimkataza kukiri kosa lake kitendo ambacho kimemfanya aendelee kusota Gerezani.

“ Hapana naona kuna shida ya maadili hapa hakuna jambo jingine Bw. TLS, nikuombe  hebu kaa na mawakili wako muliangalie hili, Kama mtuhumiwa anataka  mwenyewe kwa hiari yake kukiri  kosa lake mwacheni afanye hivyo, kwa sababu yeye ndiye anayejua ukweli wa nini alichokifanya, shaurini vizuri zingatieni maadili ya kazi zenu na taaluma zenu”. Akasisitiza  Katibu Mkuu  Mchome.

Katibu Mkuu  Mchome, ameongeza kuwa kazi kubwa ya Mawakili na Wanasheria ni kutoa ushauri wa kisheria kwa weledi, maadili mema, kwa wakati na kufanya kazi kwa matokeo  ili  haki itendeke na taifa  liendelee kupiga hatua za  maendeleo.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu  Profesa Mchome amesema, atatuma timu  ya Wanasheria  Kutoka  Wizara ya Katiba na Sheria ili kwenda kutoa msaada wa kisheria  Mkoani Kagera.

Sabaya kukata rufaa, wakili wake afunguka
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Oktoba 16, 2021