Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo imewaruhusu waliokuwa mawaziri wa serikali ya awamu ya tatu, Basil Mramba na Daniel Yona kutumikia kifungo cha nje sambamba na kufanya usafi katika maeneo ya jamii.

Mramba alikuwa Waziri wa Fedha, na Yona alikuwa waziri wa Nishati katika Serikali ya Awamu ya Tatu na wawili hao walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi na kusababishia taifa hasara ya shilingi bilioni 11.7.

Ikitoa uamuzi huo, Mahakama hiyo imeeleza kuwa haikuhusika na mchakato wa kufanikisha kifungo hicho cha nje kwa mawaziri hao bali uamuzi huo umetokana na maombi ya mawaziri hao pamoja na barua ya mapendekezo kutoka gerezani.

Hakimu Mkeha ambaye alisoma uamuzi huo, alisema kuwa Mahakama iliishinikiza barua Ustawi wa Jamii kufanya uchunguzi kufuatia majina yaliyokuwa yamependekezwa na magereza na baadae kufikia uamuzi huo.

Alisema sambamba na kifungo cha nje, mawaziri hao wa zamani wamepangiwa kutumikia adhabu ya kufanya usafi kwenye Hospitali ya Sinza Palestina kwa saa nne za kila siku.

Hakimu Mkeha alieleza kuwa masharti yaliyotumika kuwapatia kifungo hicho yalitokana na sheria ya Jamii namba 6 ya mwaka 2002, kifungu cha 3 (1).

 

“Baadhi ya vigezo vinavyotumika kwa wafungwa kutumikia adhabu ya nje ni muangalio wa ripoti yao ilikuwa inasemaje, umri, washtakiwa kama walishawai kutiwa hatiani, makosa namna yalivyo, kama wanafamilia, pia kama wanakubali kuitumikia jamii, kama wana ajira, tabia za mshtakiwa na umbali wa eneo analokaa na anapofanyia adhabu hiyo,” alisema Hakimu Mkeha.

Oktoba 2, mwaka 2015 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa uamuzi wa rufani iliyowasilishwa mahakamani hapo, na kuwahukumu mawaziri hao wa zamani kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Shilingi milioni tano, baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.

 

 

Lowassa: Magamba, 'Ufisadi' ulinitoa CCM
Msafara wa Magufuli wasimamishwa Morogoro, Awanyooshea kidole hawa