Majina ya wachezaji 22 watakaounda kikosi kitakachokwenda kushindana kuwania Kombe la Castle Cosafa nchini Afrika Kusini kimetangazwa rasmi leo Juni 14, 2017.

Akitangaza kikosi hicho kocha Mkuu wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Shabani Mayanga, amesema kinatarajiwa kuanza kambi rasmi  Jumapili Juni 18, mwaka huu. Kambi hiyo itakuwa kwenye Hoteli ya Urban Rose, iliyoko Mtaa wa Jamhuri katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Taifa Stars inajiandaa na michuano ya Cosafa inayotarajiwa kuanza Juni 25, mwaka huu. Michuano hiyo, inaandaliwa na Baraza la Mpira wa Miguu la nchi za Kusini mwa Afrika ambako Tanzania – mwanachama wa Cecafa, imepata mwaliko kushiriki.

Katika michuano hiyo, Tanzania imepangwa kundi A ambako wapinzani wake ni Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe. Timu za Botswana, Zambia na Afrika Kusini kadhalika Namibia, Lesotho na Swaziland zitakuwa na mechi maalumu (play off) ili kuingia robo fainali.

Mayanga ameweka wazi kuwa, kikosi hicho kinaundwa na makipa Aishi Salum Manula  (Azam FC), Benno David Kakolanya  (Young Africans SC) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar FC).

Wachezaji wengine ni Shomari Salum Kapombe (Azam FC) na Hassan Hamis Ramadhan ‘Kessy’ (Young Africans SC) wakati upande wa kushoto wapo Gadiel Michael (Azam FC) na Amim Abdulkarim (Toto Africans FC), Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Hassan Abdallah (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) wakati viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao (Azam FC) na Salmin Hoza wa Mbao FC.

Pamoja na viungo washambuliaji ambao ni Mzamiru Yassin Selembe (Simba), Simon Happygod Msuva (Young Africans SC), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza Ramadhani Kichuya (Simba SC), Thomas Emmanuel Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Abeid Yusufu (Kagera Sugar), Stamili Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC)

Magazeti ya Tanzania leo Juni 15, 2017
Video: Gabo Zigamba azindua filamu yake fupi ya Kisogo