Kocha mkuu wa klabu ya Simba, Jackson Mayanja ameonyesha kuridhia hatua ya kurejea kwa beki Hassan Isihaka, ambaye alikua kifungoni kutokana na utovu wa nidhamu aliouoyesha mwezi uliopita.

Mayanja, amesema mchezaji huyo sasa anaonekana kuwa amejifunza kwa kipindi chote alipokuwa nje ya timu na hali hiyo ndiyo anayoitaka iwepo kwa wachezaji wote ndani ya kikosi chake kwa kumuheshimu kocha.

Kocha huyo aliyejiunga na klabu ya Simba akitokea kwenye klabu ya Coastal Union ya jijini Tanga, ameongeza kwa kusema kuwa mchezaji anapokuwa na nidhamu ni rahisi kukaa na kocha kwa muda mrefu na kujitengenezea mazingira ya kupangwa katika kila mchezo kwa kuwa atakuwa akiyapokea vizuri maelekezo.

“Isihaka amerejea akiwa amebadilika na anaendelea na wenzake kama kawaida, lakini nikwambie kwamba mchezaji yeyote mwenye nidhamu kwa kocha wake ujue atakuwa na mafanikio makubwa hata kwa siku za usoni, lakini kama atakwenda kinyume na hapo unadhani mwalimu gani atakayethubutu kumsajili kama akijua nidhamu yake ni mbovu? Alihoji Mayanja.

Kuhusu kukosekana kwa mlinzi mwingine Abdi Banda anayesubiri maamuzi ya kamati ya nidhamu ya Simba, kufuatia kitendo cha utovu wa nidhamu aliouonyesha wakati wa mchezo wa dhidi ya Coastal Union huko jijini Tanga, Mayanja amesema kukosekana kwake hakutampa wakati mgumu kwani wapo wachezaji wenye uwezo mkubwa kuliko yeye.

Amesema hata hivyo Banda hakucheza michezo mingi iliyopita, hivyo hakumsumbui hata kidogo, huku akirejea suala la kumtumia mchezaji kutokana na nidhamu yake ndani na nje ya uwanja.

Dimitri Seluk: Man City Hawana Msimamo Kwa Yaya Toure
Uwanja Wa Old Trafford Kuongezewa Jukwaa Lenye Viti 7500