Kocha wa Simba, Jackson Mayanja, ameanza kuweka hadharani mipango ya kukisuka upya kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa 2016-17 ambao unatarajiwa kuanza mwezi August.

Mayanja ambaye alikabidhiwa kikosi cha Simba mwanzoni mwa mwaka huu, baada ya kuondolewa kwa kocha kutoka nchini England Dylan Kerr, amesisitiza kutengeneza kikosi kilichosheheni wachezaji wenye uzoefu wa kupambana.

Kocha huyo kutoka nchini Uganda, amesema anaamini wachezaji wenye kaliba ya uzoefu na ushindani ndio watakua jibu la klabu hiyo kongwe, kuondokana na matatizo ya kufanya vibaya hadi kufikia hatua ya kushindwa kutwaa ubingwa kwa mwaka wanne mfululizo sasa.

Simba ambayo mpaka sasa imeshapoteza matumaini ya kutwaa taji lolote, msimu huu ukimalizika watakuwa wanatimiza mwaka wa nne mfululizo bila ya taji la Ligi Kuu Bara huku msimu wao wa mwisho kubeba taji hilo ukiwa ni wa 2011/12.

Mayanja amesema wachezaji wazoefu ndiyo wanapaswa kusajiliwa na Simba katika kipindi kijacho cha usajili ili msimu ukianza waweze kuendana na kasi ya ligi.

“Simba inatakiwa kusajili wachezaji wengi wazoefu waliokomaa tayari na wanajua kuwa soka ndiyo kazi yao kama ilivyo kwa Yanga na Azam.

“Hali hiyo itatusaidia sana kuendana na kasi ya ligi na itatusaidia kutimiza malengo yetu ambayo tunahitaji kuyatimiza ikiwa ni pamoja na kutwaa mataji mengi,” alisema Mayanja.

Hata hivyo haifahamiki kama Mayanja ataendelea kuwepo Msimbazi kwa kipindi kingine, kutokana na uongozi wa klabu hiyo kukaa kimya mpaka sasa juu ya mustakabali wa kocha huyo ambaye aliwahi kuzinoa Kagera Sugar pamoja na Coastal Union.

Lowassa anena tena jimboni kwake
Julio Azipa Ushauri Wa Bure Simba, Young Africans