Mchambuzi wa soka la Bongo Ally Mayay ‘Tembele’ amewachambua wachezaji mahiri wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Clatous Chama na Luis Miquissone ambao kwa sasa wamekua gumzo Barani Afrika.

Wawili hao wamekua chagizo la mafanikio ya Simba SC kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hatua ya Makundi msimu huu 2020/21, huku klabu hiyo ikitinga hatua ya Robo Fainali kwa kuongoza msimamo wa ‘Kundi A’ lenye timu za Al Ahly (Misri), AS vita Club (DR Congo) na Al Merrikh (Sudan).  

Ally Mayay ambaye aliwahi kuwika na kikosi cha Young Africans na timu ya Taifa Stars, ‘Tembele’ amesema uwezo mkubwa wanaouonyesha wachezaji Clatous Chama na Luis Miquissone katika kufunga na kutengeneza mabao ni miongoni mwa sababu kubwa zinazoibeba Simba SC kwenye michuano ya kimataifa msimu huu.

“Ni suala lililo wazi kwamba Simba SC kwa sasa wapo katika kiwango bora kabisa, na hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na kuendana kwa falsafa ya timu hiyo na aina ya wachezaji walionao.”

“Falsafa ya Simba SC kwa miaka yote ni kucheza soka la kumiliki mpira na nadhani kwa sasa wamefanikiwa zaidi katika hilo kwa kuwa wana wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira kama ilivyo kwa Luis na Chama.” Amesema Ally Mayay.

Clatous Chama na Luis Miquissone wote kwa pamoja wameshatangazwa kuwa wachezaji bora wa wiki katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Makundi msimu huu 2020/21.

Luis Miquissone alitangazwa kuwa mchezaji bora wa wiki, baada ya kuonesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa mzunguuko wa pili dhidi ya Al Ahly, huku Clatous Chama akitangazwa kuwa mchezaji bora wa mzunguuko wa tano ulioshuhudia Simba SC ikishinda mabao 4-1 dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo.

Ulimwengu: TP Mazembe itakaa sawa
Rais Samia, viongozi washiriki maadhimisho ya siku ya Karume Zanzibar