Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele ameapa kuifunga Simba SC, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Jumamosi (Desemba 11).

Mchezo huo utakaounguruma Uwanja wa Benjamin Mkapa utashuhudia Young Africans wakialikwa na Simba SC kama wenyeji kuanzia mishale ya saa 11 jioni, huku Mwamuzi Henry Sasii akitangazwa kuwa msimamizi wa sheria 17.

Mayele ambaye aliitungua Simba SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwezi Septemba, amesema atahakikisha anaendeleza furaha ya mashabiki wa Young Africans katika mchezo huo wa Jumamosi (Desemba 11) kwa kuifunga tena Simba SC.

Mashambuliaji huyo amesema anajua utakuwa mchezo mgumu kwake kwa kuwa mabeki wengi wa Simba SC watamkamia, lakini atapambana kuhakikisha anatimiza wajibu wake.

Amesema ana matumaini Young Africans wanaweza kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo, ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.

“Simba SC ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri wenye majina, lakini mimi na wenzangu tumejipanga kuwafunga tena,” amesema Mayele ambaye hadi sasa ana mabao matatu kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kuelekea mchezo huo Young Africans imeweka kambi jijini Dar es salaam, huku watani zao wa jadi Simba SC wakiweka kambi mjini Lusaka Zambia, baada ya kumaliza mchezo wao wa Mkondo wa Pili wa Kombe la Shiriskiho Barani Afrika dhidi ya Red Arrows.

Shaffih Dauda aukomalia udhamini wa GSM
Aubameyang kuondoka Arsenal