Mshambuliaji Mpya wa Young Africans, Fiston Mayele, amewataka Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, kuwa watulivu na kuamini kuna kitu watakipata mwishoni mwa msimu wa 2021/22.

Mayele aliyesajiliwa na Young Africans majuma kadhaa yaliyopita akitokea AS Vita ya DR Congo, ametoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya Mashabiki na Wanachama kuzungumza vibaya kuhusu kiwango chake, baada ya kutumika kwenye mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Zanaco FC, uliomalika kwa Wananchi kufungwa mabao 2-1.

Mayele amesema: “Mashabiki wanatakiwa kuwa wavumilivu kwa sasa kwani ndio kwanza tunaanza, timu bado inaandaliwa vizuri na mwalimu, tunaamini kila kitu kitakuwa sawa.”

“Sisi kama wachezaji bado tunaendelea kupambana kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao.”

“Tunataka kuifikisha timu kwenye malengo. Wasubiri waone. Hakuna ambaye anapenda kuona timu inafanya vibaya, kama ambavyo mashabiki wanaumia pale matokeo yanavyokuwa mabaya basi na sisi wachezaji tunaumia, hivyo hatutakubali hilo litokee.”

Young Africans inaendelea kujiandaa na mchezo wake wa awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Rivers United, utakaopigwa Septemba 12, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Polepole, Gwajima, Slaa wahojiwa na kamati ya maadili ya Wabunge wa CCM
Waziri Ummy atoa maagizo kwa TARURA