Floyd Mayweather leo ametengua ahadi yake ya awali kwa Mfilipino, Manny Pacquiao akizima ndogo ya bondia huyo ya kukutana naye tena ulingoni.

Mayweather ambaye mwezi Novemba alikutana na Pacquiao nchini Japan na wakakubaliana kuwa watapigana tena, leo ametengua ahadi hiyo baada ya kumpiga Mjapan, Tenshin Nasukawa.

Akizungumza baada ya kumpiga vibaya Nasukawa kwa knockout katika raundi ya kwanza ya pambano lao la maonesho la raundi tatu, Mayweather amesema kuwa hatarajii tena kurudi kwenye ulingo wa masumbwi tofauti na alivyokuwa ameahidi kuwa angerejea rasmi Desemba mwaka huu.

“Napenda kumshukuru Tenshin. Hili pambano haliingii kwenye rekodi yetu. Bado wote ni mabingwa ambao hatujawahi kupigwa. Ni bingwa na mpiganaji mzuri,” alisema Mayweather.

“Mimi bado ni mstaafu na sitarajii kurejea kwenye masumbwi. Nilirejea kwa ajili ya kuwaburudisha watu wa Japan,” aliongeza.

Kauli hiyo itamsikitisha Pacquiao ambaye anatarajia kupigana na Andrien Broner, Januari 19 mwakani, akitegemea kuwa baada ya kushinda pambano hilo atakutana ulingoni na Mayweather kwa pambano la marudiano kama walivyokubaliana.

Mayweather alimpiga Pacquiao Mei mwaka 2015, lakini Pacquiao alidai kuwa alipigana akiwa na majeraha ya bega aliyoyapata wakati wa mazoezi. Alifanyiwa upasuaji siku chache baada ya pambano hilo, hivyo alitaka lifanyike pambano lingine kati yao.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 1, 2019
Mayweather ampiga kikatili Mjapan Nasukawa