Vita ya maneno mtandaoni kati ya bingwa wa zamani wa masumbwi, Floyd Maywether na rapa 50 Cent imechukua sura mpya baada ya bondia huyo kuwapa ajira watumiaji wa mitandao ya kijamii wenye maneno machafu.

Mayweather ambaye amembeza 50 Cent akitumia picha yake aliyokonda sana aliyopiga wakati akitayarisha filamu yake ya ‘Before I Self Destruct’ na kuweka panya wengi, amewataka matumiaji wa mitandao ya kijamii kumuandikia 50 Cent kwenye akaunti zake za kijamii maneno machafu ya kumvunjia heshima na kwamba atawalipa hadi $1,000.

Katika mashambulizi kadhaa ya matusi mitandaoni akimjibu 50 aliyeanzisha ugomvi kwa nguvu zote, Floyd amemdhihaki akidai kuwa anapaswa kugombana na saa yake mkononi na sio yeye. Floyd amenunua saa ya mkononi yenye thamani ya $18 Milioni, huku 50 Cent akikadiriwa kuwa na utajiri wa $20 Milioni.

Katika hali isiyo ya kawaida, bondia huyo pia amemrushia makombora akidai kuwa 50 ana ugonjwa wa zinaa na kwamba hivi sasa hana jipya kwenye muziki bali ameishia kuwakasirikia wachezaji na wasanii wote wanaopata mafanikio.

Hata hivyo, wawili hawa ambao walikuwa maswahiba wakubwa, wamekuwa wakigeukana mara kadhaa na kurushiana maneno makali mitandaoni lakini baada ya miezi kadhaa wanaonekana wakiwa pamoja.

Miaka minne iliyopita, wawili hawa walikuwa na bifu kali mitandaoni ambapo 50 alionekana kumzidi nguvu ya maneno Mayweather, huku akijiunga na kundi la mashabiki wa bondia wa Argentina, Marcos Maidana kwenye pambano lao la marudiano.

Hali hiyo pia imejitokeza hivi sasa ambapo Mayweather amejiunga na mashabiki wa Ja Rule akidai kuwa 50 Cent alimuibia Ja Rule mtindo wa kurap lakini hivi sasa amefuliwa.

Hata hivyo, wajuzi wa mambo wametahadharisha kuwa ugonvi wa wawili hao ni kama ugonvi wa ndugu, “wanapoanza kupigana shika jembe ukalime.”

Video: Polisi wakataa kumshtaki aliyemuua kwa risasi ‘Kijana Mweusi’
Israel yatungua ndege ya kivita ya washirika wa Urusi

Comments

comments