Bingwa wa zamani wa dunia wa masumbwi, Floyd Mayweather ametangaza kuzichapa na bingwa wa mapigano ya ngumi na mateke (kickboxing), Tenshin Nasukawa nchini Japan, Januari 31.

Mayweather ambaye hajawahi kushindwa pambano lake kati ya mapambano 50 atapanda jukwaani katika pambano lake la kurejea dhidi ya Nasukawa ambaye hajawahi kupoteza kati ya mapambano 27 ya Kickboxing na manne ya MMA/UFC.

Hata hivyo, bado wawili hao hawajaweka wazi kanuni zitakazotumika katika pambano lao kama ni kickboxing au masumbwi. Imeelezwa kuwa kanuni zitakazotumika zitawekwa wazi wiki chache zijazo.

Mayweather amechagua pambano hilo ikiwa ni pambano lake la maandalizi akisubiri pambano la marudiano kati yake na Manny Pacquiao.

“Nilitaka kufanya kitu fulani tofauti. Nilitaka kuonesha uwezo wangu nje ya Marekani na kufanya pambano la aina yake. Nilitaka kuwapa watu kile wanachotaka – ni damu, jasho na machozi,” amesema Mayweather.

Nasukawa mwenye umri wa miaka 20, ni mpiganaji aliye chini ya kampuni ya RIZIN Fighting Federation ambayo imeingia mkataba na Mayweather, inayojihusisha na mapigano ya kickboxing na martial arts.

“lilikuwa dili la kunishangaza lakini nilikubali bila kusita. Ni tukio kubwa zaidi katika maisha yangu na nataka kuwa mwanaume ambaye amebadili historia. Nitafanya hivyo kwa kutumia ngumi hizi, kwa konde moja, nyie angalieni tu,” alisema Nasukawa.

Mwaka jana, Mayweather alifanikiwa kumpiga Conor McGregor kwenye pambano lao lililoingiza fedha nyingi.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Novemba 6, 2018
Revocatus Kuuli afungiwa maisha, Young Africans kuchaguana Januari 13

Comments

comments