Msuluhishi wa mgogoro wa kisiasa wa Burundi Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamini Mkapa, ameanza mazungumzo ya suluhisho la mgogoro wa Burundi ambayo yanafanyika jijini Arusha nchini Tanzania.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho Rais mstaafu, Benjamin Mkapa amesema kuwa hadi sasa jitihada zake za kuishawishi serikali ya Burundi kuhudhuria kikao hicho hazijafanikiwa.

Amesema kuwa mjadala huo utaendelea na ataendelea kutimiza jukumu alilopewa na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki

Aidha, Mkapa amewataka washiriki wa mazungumzo hayo kuwa huru kujadili na kutoa mapendekezo yao wanayo amini kuwa yataweza kuleta amani ya kudumu katika taifa la Burundi na kuhakikisha kuwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka 2020 kuwa ni huru na wa haki.

Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani akiwemo mwenyekiti wa CNDD amesema kuwa kutoshiriki kwa serikali ya Burundi kuna wakatisha tamaa ya kupatikana kwa kile walichotarajia.

Mgogoro wa kisiasa katika nchi ya Burundi ulianza mwaka 2015 kufuatia uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ambao licha ya kuwa ulifanyika hali ya amani, vitisho na vurugu viliendelea kuiandama nchi hiyo hatua iliyopelekea Umoja wa Afrika kuingilia kati na kuagiza jumuiya ya Afrika Mashariki kutatua mgogoro huo .

 

Serikali yamkaanga Wema Sepetu
Kambi ya Taifa Stars yapangua tena ratiba ligi kuu