Klabu ya Mbao FC imetoa angalizo kwa wachezaji watakaotemwa kwenye klabu kongwe za Simba SC na Young Africans kutotarajia kusajiliwa na wanafainali hao wa michuano ya kombe la shirikisho kwa mwaka 2017.

Mbao FC, ipo katika mchakato wa kufanya usajili wa baadhi ya wachezaji watakao kiongezea nguvu kikosi chao kwa ajili ya msimu mpya wa ligi kuu ambao umepangwa kuanza mwezi Agosti mwaka huu.

Afisa habari wa Mbao FC Cristant Malinzi, amezungumza na Dar24, na kusema lengo la Mbao FC ni kufanya usajili makini bila kufuata mkumbo wa kuangalia nani alikua wapi kwa msimu uliopita, tena kwa kufuata kigezo cha klabu kongwe hapa nchini.

“Naomba niseme kabisa kuhusu hili, hatutofuata utaratibu wa baadhi ya klabu za soka hapa nchini ambazo kila msimu zimekua zikiwapapatikia wachezaji wanaotemwa na klabu za Simba na Young Africans,”

“Mbao FC tunaamini wachezaji wasiokua na majina ndio wenye uwezo mkubwa wa kutaka kucheza soka ili wafikie malengo yao, na sio wanaotemwa katika klabu kongwe,”

“Katika soka la Tanzania hakuna daraja la juu katika uchezaji zaidi ya Simba na Young Africans, sasa mchezaji kama anatemwa katika klabu hizo atakua na kiwango cha soka?” Alihoji Cristant Malinzi.

Wakati huo huo Malinzi amekiri kuondoka kwa beki wao wa pembeni Jamal Mwambeleko anaeripotiwa kujiunga na klabu ya Simba ya Dar es salaam.

Malinzi amesema mchezaji huyo amemaliza mkataba wa kuitumikia Mbao FC na alifanya mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo ya jijini Mwanza, lakini hakufikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya, hivyo wakaona ni bora wampe baraka za kuondoka na kwenda kusaka maslahi mahala pengine.

Akamatwa kwa kumshawishi mpenzi wake ajiue kisha achangishe fedha mtandaoni
Ushangiliaji Wamponza Federico Valverde