Kikosi cha Mbao FC kimeanza maandalizi ya mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Azam FC, ambao umepangwa kuchezwa jijini Dar es salaam mwishoni mwa juma hili katika uwanja wa Azam Complex.

Mbao FC wamerejea mazoezini, baada ya kuibanjua Young Africans bao moja kwa sifuri katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la shirikisho, mwishoni mwa juma lililopita kwenye uwanja wa CCM Kirumba.

Afisa habari wa Mbao FC Crinstant Malinzi amezungumza na Dar24 na kueleza mipango ya maandalizi yao kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam FC.

Amesema kikosi chao kipo katika hali nzuri na kila ari kubwa ya kufanya vizuri dhidi ya Azam FC siku ya jumamosi.

“Tupo katika ari kubwa ya kuamini hakuna kitakachoshindikana jumamosi, nikuhakikishie tu, Mbao FC ipo kwa ajili ya kupambana na yoyote, hatuna hofu ya kupambana na Azam FC.”

“Kitendo cha kuifunga Yanga, kimetuongezea morari kubwa, na ninaamini hii itatusaidia sana katika mchezo wetu ujao dhidi ya Azam FC, tunatambua tupo katika mazingira ya kuepuka kushuka daraja na wakati mwingine suala hili limekua chachu kwetu kuendelea kuhimizana ili tufanye vyema kwenye michezo ya ligi iliyosalia.” Amesema Malinzi.

Mbao FC inatarajia kusafiri hadi jijini Dar es salaam siku ya Al-khamis kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam FC.

Picha: JPM amaliza ziara Kilimanjaro, arejea Dar es salaam.
Video: Serikali kushughulikia huduma bure za afya wenye ulemavu