Jeshi la Polisi mkoani Tabora linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukamatwa na vitu mbalimbali vya wizi yakiwamo mafuta ya maiti ya binadamu yaliyokuwa ndani ya chupa ya plastiki ya lita moja.

Kamanda wa polisi mkoani Tabora, Emanuel Nley ametaja majina ya watuhumiwa hao kuwa ni Sued Haruna Bakari (49) mkulima, mkazi wa sikonge, na Mani Sabasaba (47), mkazi wa Ifakara mkoani Morogoro.

Watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na msako mkali ulofanywa na jeshi la polisi mkoani humo katika Wilaya zake zote saba.

Kamanda Nley amesema baada ya kukamatwa na kupekuliwa walikutwa na bastola ndogo namba 375, gobore isiyo na namba pamoja na mafuta ya maiti.

Ameeleza kuwa baada ya kubanwa na polisi waeleze mafuta hayo ni ya nini walisema ni ya maiti ya binadamu na walikuwa wakiyatumia kwa imani za kishirikina kufanikisha mambo yao, na kwamba uchunguzi wa kina utafanyika ikiwemo mafuta kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Nakusisitiza kuwa baada ya uchunguzi huo, itakapobainika pasipo shaka kuwa mafuta hayo ni ya maiti ya binadamu, wataeleza walikoyapata na waliyapataje.

Aidha Kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili hatua ziweze kuchukuliwa haraka iwezekanavyo.

Kipigo cha mwalimu champofusha mwanafunzi
Johari kuzindua filamu siku ya Idi Mosi Mbeya