Jumla ya watu 72 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma kwa tuhuma mbalimbali, likiwemo tukio la uwindaji haramu na kukutwa na nyara za Serikali zenye jumla ya thamani ya shilingi 2,875,000.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo, Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma Gilles Muroto, amemtaja mtuhumiwa mfanyabiashara Jonathan Dastan Temu (41), aliyekutwa akiwa na nyama ya wanyama pori aina ya Nsya wanne na Digidigi mmoja.

“ Bado tunafuatilia silaha iliyotumika katika kutekeleza tukio hili la uwindaji haramu, lakini mtuhumiwa tayari yuko mikononi mwa Polisi na atafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kufanyika hivyo tunaomba ushirikiano kwa hili.” Amefafanua Kamanda Muroto

Amesema mbali na tukio hilo, pia Polisi wanawashikilia Madereva watano waliokuwa wakisafirisha Abiria na mafuta kwa njia ya hatarishi lita 1,277 za Petrol na lita 850 za Diesel, sambamba na watuhumiwa wengine wanne walioshirikiana nao na kufanya jumla yao kufikia watu tisa.

Kamanda Muroto amewataja madereva hao kuwa ni Richard Ng’olo (52) na Nicholaus Kasiri (28), wakiwa na Basi aina ya Scania lenye namba za usajili T 509 ACV na Sixtus Salvatory Ombay (39) akiwa na gari aina ya Toyote Coaster lenye namba za usajili T 493 DPA.

Wengine ni Jairos Simba (52) na Anicet Hoya (23) wakiwa na Basi aina ya Scania lenye namba za usajili T 783 ASY, Shaban Shaban (34) na Benson Mpali (34) wakiwa na gari aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T 733 DNY na Paulo Kwaslema (32) na Kashindye Maganga (29) wakiwa na gari aina ya TATA lenye namba za usajili T 637 DGN.

“Mnaweza mkajionea katika hili yaani gari ya abiria inapakia mafuta ya vyombo vya moto na Abiria kwa pamoja hii ni hatari sana, lengo letu si kuzuia huu usafirishaji ila watumie njia zilizo salama, watu hawataki kujifunza kwa yaliyotokea sehemu mbalimbali jinsi ndugu zetu walivyopoteza maisha kwa ajali za moto hatutaruhusu hili.” Ameongeza Muroto

Aidha Kamanda Muroto amesema wanawashikilia watuhumiwa wengine kwa makosa ya upatikanaji wa vifaa vya kuvunjia nyumba, biashara ya ukahaba, upatikanaji wa mirungi, pombe ya moshi, bangi, mali ya wizi na unyang’anyi wa kutumia nguvu.

Amebainisha kuwa katika tuhuma za unyang’anyi wa kutumia nguvu, wanawashikilia watuhumiwa tisa na pikipiki nne zenye namba za usajili MC 154 BYG Boxer, MC 660 AXD Boxer, MC 223 Haojue na MC 569 BMZ Haojue wanazozitumia kutekeleza uhalifu huo.

“Hawa watu usiku ndio wanafanya huu uhalifu, unaweza kujionea pikipiki zao wanafunga manati na wanaweka vitambaa nyuma kwa lengo la kuficha namba baada ya tukio, tunawaambia kwamba msako utaendelea na tutawakamata kokote walipo.” Amesisitiza Muroto.

Kufuatia matukio hayo, Kamanda huyo wa Polisi Mkoani Dodoma amewataka wananchi na mamlaka mbalimbali ikiwemo Ewura kutoa ushirikiano katika kuwabaini, kuwafichua na kuwachukulia hatua mbalimbali ili kuweza kukomesha uhalifu.

Marekani: Ndege yaahirisha safari baada ya Wanaume kupungiana Mikono
Fatma Karume ajibu tuhuma za kusimamishwa Uwakili, 'Mimi bado wakili'