Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR – Mageuzi) amepinga uamuzi wa Bunge kuwapa adhabu mfululizo wabunge wa Upinzani akisema kuwa uamuzi huo utaongeza mpasuko Bungeni.

Mbatia amesema kuwa ingawa kuna kanuni na taratibu za Bunge zinazotoa nafasi ya adhabu, kutokana na hali ya Bunge ilivyo sasa, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson hakupaswa kuridhia adhabu ya wabunge wawili wa Chadema, Susan Lymo na Anatropia Theonest.

Jana, Naibu Spika alitangaza adhabu ya kuwasimamisha wabunge hao wa Chadema baada ya Kamati ya Maadili kubaini kuwa walilidanganya Bunge.

“Ni hatari kuona Bunge linatumika kama idara inayoongozwa na Serikali. Dk. Tulia hakupaswa kuridhia adhabu hiyo kwa sababu inaongeza mpasuko,” Mbatia aliwaambia waandishi wa habari na kuongeza kuwa kunapokuwa na migogoro katika mhimili huo ni vigumu kupanga na kuwaletea maendeleo wananchi ipasavyo.

Kwa upande wa wabunge wa CCM kwa nyakati tofauti, wao waliunga mkono uamuzi huo wa Naibu Spika na kueleza kuwa Bunge lina kanuni zake ambazo ni lazima zifuatwe na wabunge wote ili kuepuka hatua kama hizo.

“Muhimu zaidi ni kufuata kanuni za Bunge, maisha ya Bunge yanakuwa rahisi sana na kanuni zimerahisisha na zimeweka wazi jambo hilo. Lakini ukienda kinyume cha kanuni basi adhabu zipo,” alisema Mbunge wa Bukene, Selemani Zedi (CCM).

Belle 9 kuwapa zawadi nzito mashabiki wake, yuko tayari kushuka WCB
Utapenda jibu la Oprah kwa Donald Trump baada ya kumuomba awe mgombea mwenza wake

Comments

comments