Siku moja baada ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kudai Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ni miongoni mwa wadaiwa sugu wa shirika hilo na amepewa notisi ya kuondoa biashara yake kwenye Jengo la Bilicanas liliko Posta jijini Dar es Salaam, Mbowe amejitokeza na kukana taarifa hizo.

Jana Mkurugenzi wa NHC, Nehemiah Mchechu aliitaja kampuni ya Mbowe Hotels ambayo Mwenyekiti huyo wa Chadema ni mmoja wa wamiliki, kuwa wameshapewa notisi ya kuhama jengo hilo baada ya mwezi huu.

Kupitia Twitter, Mbowe amekana kudaiwa na shirika hilo na kwamba kinachofanywa ni sehemu ya kumuadhibu kutokana na ushiriki wake kwenye siasa.

“Hivyo, ningependa umma wa Watanzania uelewe kuwa sidaiwi na Shirika la Nyumba la Taifa(NHC). Kufuatia utata huu wanasheria wa Kampuni wanashughulikia jambo hili kwa taratibu za kibiashara na kisheria,” Mbowe ameandika.

Ameeleza kuwa kwa muda mrefu kulikuwa na mgogoro wa kimkataba kati ya kampuni hiyo na NHC lakini kampuni hiyo imekuwa ikilipa kodi stahiki kwa mujibu wa mkataba husika.

“Wafanyabiashara wengi wanafungwa fikra na midomo ndani ya nchi hii kwa kuogopa hila na ghiliba za watawala. Ni heri kufa masikini nikiwa nimesimamia ukweli, kuliko kuishi tajiri niliyetawaliwa na ubinafsi, woga, hofu na ubatili,” aliandika.

Hata hivyo, jana Mchechu alisisitiza kuwa hatua ya shirika hilo haina uhusiano wowote na masuala ya kisiasa.

Jeshi la Polisi kuwasaka wanaolibeza na kushabikia uhalifu mitandaoni
Video: Ukawa, ACT-Wazalendo washauri Rais Magufuli afute vyama vyote vya siasa