Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kuwa chama hicho kilishiriki kikamilifu katika ajali ya MV. Nyerere, hivyo tuhuma zilizotolewa na aliyekuwa Mbunge wa chama hicho katika jimbo la Ukerewe kuwa chama hicho kilimtelekeza wakati wa msiba si za kweli, akidai kuwa chama hicho kilimpatia rambirambi mbunge huyo.

Mbunge Joseph Mkundi aliandika barua kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai akieleza kujiuzulu uanachama wa CHADEMA, udiwani pamoja na ubunge wa jimbo lake kwa madai ya chama chake kukosa utu kwa kumtelekeza katika wakati wa majonzi.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa mahojiano na East Africa Radio, ambapo Mbowe amedai kuwa maneno ya mbunge huyo katika barua ya kujiuzulu ni tofauti na taarifa aliyoitoa katika kipindi cha msiba ambapo alieleza kuwa chama chake kipo bega kwa bega na yeye.

“Imekuwa kawaida kwa kila anayehama anatoka na sababu zake za kitoto, kama yeye anasema hakupewa ushirikiano na wakati awali katika taarifa yake alisema anatambua mchango wa chama katika msiba ule lakini, kama viongozi wa chama wa kanda ya ziwa wote walikuwepo labda yeye aseme alitaka sura gani ifike pale ndio ajue kuwa chama chake kiliungana nae,” amesema Mbowe.

Alipoulizwa sababu ya yeye kutofika eneo la tukio, alikata simu na hakupokea tena alipopigiwa mara nyingine.

Aidha, katika barua yake kwa Spika wa bunge, Mkundi medai kuwa Chama chake cha zamani (CHADEMA) kimepoteza heshima na utu baada ya kumtelekeza katika kipindi ambacho alihitaji msaada na ushirikiano kutoka kwenye chama hicho na uongozi wake katika kipindi cha msiba wa ajali ya Kivuko cha MV. Nyerere, iliyotokea Septemba 20, 2018.

Hata hivyo, Joseph Mkundi anakuwa Mbunge wa tano kutoka CHADEMA kuhama na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi kwa kile wanachodai kuwaletea wananchi maendeleo akiungana na Mwita Waitara, Julius Kalanga, Chacha Marwa Ryoba na Godwin Moleli.

 

Aaron Ramsey bado kizungumkuti Arsenal
Serikali kuimarisha matumizi ya Fukwe

Comments

comments