Siku chache baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa kutangaza rasmi kumuunga mkono mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, Mwenyeti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza kuwa bado ana nafasi ya kurudi Chadema.

Akiongea katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika katika wilaya ya Karatu, Mbowe alitaja mambo mbalimbali aliyofanya na Dk. Slaa katika harakati za kukiimarisha chama hicho kwa lengo la kushika dola huku akimtaja kuwa alikuwa mtu mkweli hadi alipobadilishwa na matakwa ya mkewe, Josephine.

Katika maelezo yake wakati akisimulia uhusiano wake na Dk. Slaa ambaye alimuita rafiki yake na msiri wake, Mbowe alieleza kuwa awali walikubaliana na Dk. Slaa kuhusu kumchukua Lowassa kutoka CCM endapo jina lake ‘litakatwa’, lengo likiwa kuibomoa CCM kama walivyokuwa wameshauriwa na wataalam kutoka Marekani na Afrika Kusini waliowapa kazi ya kufanya utafiti kuhusu uwezekano wa kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Alisema kuwa baada ya wataalam hao kukamilisha utafiti wao waliwapa majibu ambayo hayakuwa mazuri kwa upande wao na ndipo wakakubaliana njia mbadala kwa kuwa ilionekana dhahiri kuwa Dk. Slaa asingeweza kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu bila kuibomoa CCM.

Mbowe alisimulia kile alichokiita mpango wa siri ambao hakuwahi hata kumwambia Lowassa baada ya kuingia Chadema.

“Majibu hayakuwa mazuri na Dk. Slaa alijua, wakatuambia Chadema mna nguvu lakini hauwezi kuwa na nguvu mkiacha CCM salama, wakasema tufanye juu chini, tukeshe tukiomba CCM isiingie kwenye uchaguzi ikiwa imara. Wakatushauri, ‘pasueni CCM’. Hili hata Lowassa sijamwambia, katika utafiti ule tuliambiwa atakayetusumbua akiwa CCM ni mtu mmoja tu, ni Lowassa.

“Wakatuambia mkiwa na mgombea wenu Dk. Slaa, na Lowassa akawa CCM ana watu CCM na ndani ya Chadema watamuunga mkono. Siku hiyo tulikaa na Dk. Slaa tukiangaliana kwa dakika 10 hakuna kuongea,” alisimulia.

Alisema kuwa wote walikubaliana kuwa endapo Lowassa atakatwa na CCM wamchukue ili agombee kupitia Chadema, lakini matakwa ya mke wa Dk. Slaa yalipelekea mwanasiasa huyo kushindwa kusimamia makubaliano hayo mwishoni.

Hata hivyo, Mbowe alimfungulia milango tena Dk. Slaa na kueleza kuwa watampokea tena endapo ataamua kuachana kuiunga mkono CCM kwa kuwa bado anaamini uwezo wake na mchango wake ndani ya chama.

“Dk. Slaa akiona wakati wowote bado kuna nafasi na akijisikia kuja tumpokee, kama ataona watu wote ambao ni kinywa cha Mungu ila yeye na mkewe ndio wako sawa tumsamehe twende mbele. Tuliamua tumkamate Lowassa na tayari ameisaidia Chadema,” alisema.

 

 

Sumaye Aweka Tena Richmond Mezani
CCM Walia Na Picha Za Mikutano Ya Lowassa