Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amemtumia ujumbe Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kuhusu uamuzi wa kumvua Tundu Lissu ubunge wa Singida Mashariki.

Akizungumza leo katika kikao cha ndani cha chama hicho kilichofanyika Kanda ya Nyasa, Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni alisema kuwa hatua hiyo haiwezi kuwavunja moyo bali inazidi kuwaimarisha hata kama wabunge wao wote wataondolewa.

“Yaani spika leo anamfukuza ubunge Lissu anadhani tutalia, tunamwambia Mheshimiwa Spika acha Lissu chukua viti vyote hivi, nani ana shida na ubunge, sisi tuna shida na wananchi,” amesema Mbowe.

Mbunge huyo wa Hai ameongeza kuwa hatua hiyo imewapa hasira ambazo watazihamishia katika kuhakikisha wanaingiza wabunge wengi zaidi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na kuondoa wingi wa wabunge wa Chama cha Mapinduzi.

Spika Ndugai alifafanua kuwa amemtaarifa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa jimbo la Singida Mashariki liko wazi kwakuwa aliyekuwa Mbunge wake, Lissu amevunja taratibu na kanuni kwa kutohudhuria vikao kadhaa vya bunge bila kutoa taarifa na kushindwa kujaza fomu ya maadili.

Alieleza kuwa amekuwa akimuona kwenye vyombo vya habari akizunguka nchi mbalimbali na kufanya mikutano lakini hahudhurii vikao vya bunge wala kutoa taarifa zenye sababu ya kutohudhuria vikao hivyo, kinyume cha kanuni na sheria husika.

Vijana wengi zaidi Tanzania hatarini kupata ugonjwa wa kiharusi
LIVE: Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT)