Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameweka wazi wanufaika wa harakati na mapambano ya kuingia ikulu yanayofanywa na aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho, Edward Lowassa.

Akizungumza jana katika hafla ya shukurani iliyofanyika nyumbani kwa Lowassa, Masaki Jijini Dar es Salaam, baada ya ibada maalum ya shukurani iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Azania Front, Dar es Salaam, Mbowe alisema kuwa sio lazima mwanasiasa huyo mkongwe aonje mwenyewe matunda ya kazi kubwa aliyoifanya bali hata kizazi kijacho.

“Kazi anayofanya Lowassa (Baba Kadeti) si lazima aone matunda yake leo, huenda mtoto wake ataonja na asipoonja Kadeti basi wajukuu wataonja matunda hayo na kutambua mchango mzuri wa babu yao kwa kazi kubwa ya maana anayofanya sasa,” amesema.

Akizungumza mbele ya watu takribani 600 waliohudhuria hafla hiyo wakiwemo watu wake wa karibu waliomuunga mkono wakati wa kampeni za mwaka jana, Mbowe aliwataka wale wote waliokuwa na matarajio ya kushinda katika uchaguzi uliopita kutokata tamaa kwani uchaguzi sio tukio bali ni mchakato unaoendelea.

Alisema kuwa wanaoshiriki katika harakati za siasa za chama hicho wakiwa kwa maslahi binafsi wanapaswa kujitafakari kwani kuna kazi kubwa inayofuata katika chaguzi zijazo.

Akizungumza awali, Mke wa Waziri Mkuu huyo Mstaafu, Mama Regina Lowassa alisema kuwa familia hiyo ina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa mengi waliyoyapitia na namna anavyowalinda na kwamba ndio sababu wameamua kufika kanisani kumshukuru.

“Tumepata mengi mazuri, tunaweza kusafiri kwenda Monduli na kurudi si sababu tuna magari mazuri kuliko wengine; tunaweza kusafiri kwa ndege na tukarudi salama, lakini hata wakati mwingine unasikia mtu anakupigia simu kukusalimu au kukuandikia ujumbe mzuri wa faraja, haya yote  ni sababu ya Mungu na tukaona leo tufike Kanisani kusema Mungu asante kwa mema yote uliyotujalia,” alisema alisema Mama Lowassa.

 

Kifo Cha Johan Cruyff Kuleta Mabadiliko Ya Uwanja Wa FC Barcelona
Magufuli aongezewa orodha ya majipu