Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewataka vijana wanaounda Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) kusitisha azimio lao la kukutana mjini Dodoma kwa kile walichodai kusaidia Polisi kuzuia mkutano wa Mkuu Maalum wa CCM.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Arusha, katika mkutano wa Mameya na Wenyeviti wa halmashauri 18 zinazoongozwa na Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa), Mbowe alisema kuwa amechukua uamuzi huo ili kuzuia madhara yatakayojitokeza.

Alisema kuwa ingawa wamesitisha mpango huo, tayari wamefanikisha kuionesha dunia jinsi ambavyo Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi kwa kuvunja sheria na kwa upendeleo.

“Wakati sisi tunazuiwa kufanya siasa, Rais anafanya siasa, Waziri Mkuu anafanya siasa, mawaziri wanafanya siasa, wakuu wa mikoa na wilaya wanafanya siasa jambo ambalo si sahihi,” alisema Mbowe.

Alisema kuwa wakati Polisi wanatoa ufafanuzi kuwa hawakukataza mikutano ya ndani, tayari wameshazuia mikutano kadhaa ya ndani ya Chadema ikiwa ni pamoja na mahafali za wanafunzi wa vyuo vikuu, wakati CCM wakiendelea kufanya mahafali.

Mwenyekiti huyo aliwataka BAVICHA kuwa watulivu na wasubiri maelekezo mengine kutoka ngazi ya juu ya chama hicho. Alisema hivi sasa chama kitaendelea kujikita katika kufanya mikutano ya ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Mbowe alilitaka Jeshi la Polisi kuwaachia mara moja viongozi wa BAVICHA waliokamatwa mjini Dodoma. Alidai kuwa wamepata taarifa Jeshi hilo limepanga kuwashikilia hadi mkutano huo wa CCM utakapomalizika.

Dk. Tulia afunguka kuhusu hatima yake na wabunge wa Ukawa
Ureno yatwaa kombe la Ulaya, yaacha kilio Ufaransa