Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wameshinda rufaa iliyofunguliwa Mahakama ya Rufani na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kupinga kusikilizwa kwa maombi ya kupewa dhamana.

Mahakama hiyo ya Rufani imetoa uamuzi wake leo na kutupilia mbali maombi ya DPP ya kuitaka kufuta uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutaka kuendelea kusikilizwa kwa maombi ya kupinga kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Katika rufaa hiyo, DPP alieleza kuwa Mahakama Kuu katika uamuzi wake ilikiuka sheria na kwamba hakupewa nafasi ya kutosha kusikilizwa.

Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai pamoja na Matiku walikata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuwafutia dhamana baada ya kukosa kufika Mahakamani kwa ajili ya kesi ya jinai inayowakabili.

DPP aliiomba Mahakama Kuu kutokubali kusikiliza maombi hayo ya Mbowe na Matiku lakini Jaji Sama Rumanyika alitupilia mbali pingamizi hilo na kupanga tarehe ya kuanza kusikiliza. Hivyo, DPP alikata rufaa mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo.

Hatua hiyo imetoa mwanga kwa wabunge hao wa upinzani kujaribu bahati yao kupitia sheria kuomba mahakama ifute uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ili waweze kupata dhamana wakati kesi yao ya msingi ikiendelea.

 

DC Mtwara aagiza kuadhibiwa kwa Watumishi
Majaliwa awaonya wafanyabiashara kuhusu rushwa