Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wengine saba waandamizi wa chama hicho wamekata rufaa Mahakama Kuu wakipinga adhabu iliyotolewa dhidi yao na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Machi 10, 2020, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliwahukumu Mbowe na wenzake kulipa faini ya jumla ya Sh. 350M/- au kwenda jela miezi 60 kwa jumla baada ya kuwakuta na hatia ya uchochezi na kufanya mkusanyiko usio halali.

Mahakama ilieleza kuwa mashtaka na ushahidi uliotolewa na Mwanasheria wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ulithibitisha pasipo na shaka yoyote kuwa walitenda makosa hayo. Mahakama iliwakuta na hatia katika mashtaka 12 kati ya 13.  

Jana, Wakili wa viongozi hao wa Chadema, Peter Kibatala alimuomba Jaji Ilvin Mgeta wa Mahakama Kuu kuwa Mahakama hiyo iwafutie wateja wake kifungo kilichotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

“Hakukuwa na uchambuzi yakinifu uliotolewa na Mahakama kuhusu mashtaka dhidi ya wakata rufaa, kwa kulinganisha na ushahidi/vielelezo vilivyowasilishwa,” alisema Kibatala na kuongeza kuwa Mahakama haikutenda haki kukubali vielelezo vya picha za video na sauti kinyume na sheria inayotoa muongozo wa jinsi ya kutumia ushahidi wa kielektroniki.

Pia, Kibatala aliieleza Mahakama Kuu kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi haikuzingatia uhalisia kuwa baadhi ya mashtaka dhidi ya wateja wake hayakuwa na uhalisia kwani vitendo vinavyodaiwa kufanywa na watu hao vinatajwa katika mazingira ambayo hawakuwepo wakati huo (alibi).

Viongozi wa Chadema waliohukumiwa na kukata rufaa mbali na Mbowe, ni pamoja na John Mnyika (Katibu Mkuu), Salum Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar) na Peter Msigwa (Mbunge wa Iringa).

Haji Manara apandisha mzuka, arudisha majibu
Serikali yafungua anga la Dar, ndege kutoka nje rukhsa