Mbunge wa Jimbo la Konde Kisiwani Pemba, Khatib Haji wa Chama cha ACT Wazalendo, amefariki Dunia alfajiri ya leo Mei 20, 2021 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.

Kifo cha Mbunge Haji kimethibitishwa na Katibu Idara ya Bunge Baraza la Wawakilishi na Serikali za Mitaa, Hamad Yussuf leo Mei 20, 2021.

“Nasikitika kuwatangazia Kifo cha Mhe Khatib Said Haji Mbunge wa Jimbo la Konde, ambaye umauti umemfika akiwa anapatiwa Matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili Alfajiri ya leo, mipango ya mazishi inaendelea na tutajulishwa baadae kidogo.

Kwa Niaba ya Idara ya Bunge, Baraza la Wawakilishi na Serikali za Mitaa natoa pole kwa Kiongozi wa Chama na Viongozi wengine wote, Familia na Wananchi wa Jimbo la Konde, Allah amsamehe makosa yake, ampe kauli thabiti ampe pepo ya Firdaus na sisi atujaalie mwisho mwema Aamin,” ameeleza Yussuf.

Khatibu aliwahi kuwa Mbunge wa Konde kupitia Chama cha Wananchi CUF mwaka 2010 hadi 2020, alishawahi kushika nafasi ya Waziri wa Kilimo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mwaka 1984 hadi 1987.

Aidha, alikuwa ni miongoni mwa wabunge ambao hivi karibuni walizua gumzo bungeni baada ya kudai kuwa, mahabusu wa Uamsho wanamliza kutokana na uwepo wa mahabusu hao kwa muda mrefu gerezani Tanzania Bara na kuiomba Serikali ifanye uamuzi wa busara ili kuona wanapewa haki ya kuachiwa huru.

Katika Bunge hili la 12, Khatib amekuwa Mbunge wa tatu kufariki tangu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020. January 21 2021 Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Manyara, Martha Umbulla alifariki dunia na Februari 12, 2021 Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, Mkoa wa Kigoma Atashasta Nditiye alifariki Dunia baada ya kupata ajali ya gari.

Majaliwa ataka hatua zaidi zichukuliwe wanaohusika na mfumo wa LUKU
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Mei 20, 2021