Siku chache baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza kuwahoji baadhi ya wabunge wanaounda Kamati mbalimbali za Bunge, mbunge mmoja amefunguka namna walivyoitiwa ‘mlungula’ na taasisi moja ya umma.

Mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, ni mmoja kati ya wabunge waliohojiwa na Takukuru hivi karibuni ambapo hakutaka jina lake litajwe hadharani, lakini alikiri kuitiwa ‘rushwa’ iliopewa jina tamu la kuipunguzia ukali.

“Nilikuwa kwenye majukumu yangu, nilipoambiwa kuna ‘Lunch’, yaani fedha kutoka kwenye moja ya idara tulizokuwa tunazikagua, niliwasilana na Katibu wa kamati yetu nikamuuliza kama jambo hilo lipo sawa na akanishauri nisishiriki,” Mbunge huyo aliliambia gazeti moja la kila siku.

Sakata hilo la rushwa kwa wajumbe wa kamati za Bunge zinazokagua mashirika na taasisi za umma lilipelekea Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe kujiuzulu nafasi zao wakishinikiza kufanyika kwa uchunguzi na kulisafisha Bunge.

Hata hivyo, wakati Takukuru wanaendelea na kazi yao ya uchunguzi na kuwahoji wabunge, Spika wa Bunge tayari ameshapangua safu ya Wenyeviti na Wenyeviti wasaidizi wa Kamati Mbalimbali za Bunge.

 

Makonda kuwakamata watakampa taarifa kuhusu Rushwa makanisani
Wanajeshi wa JWTZ wabanwa na Polisi kwa kipigo, mauaji